Maoni: Afrika Mashariki bado yanuka ufisadi | Matukio ya Afrika | DW | 05.12.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Maoni: Afrika Mashariki bado yanuka ufisadi

Katika orodha ya nchi 176 zilizofanyiwa utafiti wa shirika la kimataifa la kupambana na ufisadi, Transparency International, nchi tano zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki hazimo hata kwenye kumi bora.

Utaratibu uliotumiwa na Faharasa ya Transparency International, ni kwamba nchi zilizopata alama kuanzia 50 kwenda juu, zinahisabiwa kuwa zipo kwenye nafasi nzuri kwenye mapambano yake dhidi ya ufisadi, wakati zile zilizopata alama 49 kushuka chini, zinahisabiwa kufanya vibaya kwenye mapambano hayo.

Na Mohammed Khelef

Na Mohammed Khelef

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na hata taifa jirani na kubwa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, zote kwa pamoja ziko chini ya alama 49, ikimaanisha kwamba ziko kwenye hali mbaya sana kwa ufisadi, ingawa zinapishana kwa ubaya huo.

Kwa mfano, Burundi ambalo ndilo taifa lenye uchumi mdogo zaidi kwenye eneo hilo, ndiyo ya mwisho kwa kupata alama 19, ikimaanisha kwamba inaongoza kwa ufisadi miongoni mwa mataifa ya Afrika Mashariki, ikishikilia nafasi ya 165 duniani.

Kenya, ambalo ni taifa lenye uchumi mkubwa zaidi kwenye eneo hilo, imepata alama 27 ikimaanisha kuwa iko kwenye hali mbaya katika nafasi yake ya 139 duniani, ikipitwa hata na Uganda iliyo nafasi ya 130 ikiwa na alama 29 na Tanzania iliyo na alama 35 katika nafasi ya 102 miongoni mwa mataifa 176 duniani.

Hata hivyo, Rwanda inasimama kama doa jeupe kwenye kuku mweusi. Inaweza kuambiwa ina afadhali kidogo. Licha ya udogo wake kieneo, kwa idadi ya watu na hata uchumi, Rwanda imeshika nafasi ya 50 ikiwa na alama 53.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, taifa ambalo si mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini linalopakana na mataifa manne ya eneo hilo – Tanzania, Uganda, Burundi na Rwanda – iko kwenye nafasi 160 ikiwa na alama 21.

Mataifa 10 yaliyo bora zaidi kwenye mapambano hayo ni Denmark, Finland, New Zealand, Sweden, Singapore, Switzerland, Australia, Norway, Canada na Uholanzi. Wakati mataifa 10 yaliyo na kiwango kikubwa zaidi cha ufisadi ni Haiti, Venezuela, Iraq, Turkmenistan, Uzbekistan, Myanmar, Sudan, Afghanistan, Korea ya Kaskazini na Somalia.

Licha ya kuwa mataifa ya Afrika Mashariki hayamo kwenye mataifa 10 ya mwisho kabisa, lakini pia hayamo kwenye mataifa 10 ya mwanzo kabisa katika kupambana na ufisadi. Maana yake ni kwamba mtu anayeishi Afrika Mashariki ana uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa fisadi kuliko wanaoishi kwenye maeneo mengine ya dunia, ambako alama za kuwajibika kwa jamii na serikali zao dhidi ya rushwa ni kubwa.

Wakati viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakipigania kuelekea kwenye shirikisho la kisiasa japokuwa hata la kiuchumi walilonalo sasa halijatangamaa, ukweli mchungu ni kwamba eneo hilo linanuka ufisadi.

Rwanda inaonesha mafanikio makubwa, kwani imezipita hata nchi zenye uchumi mkubwa kama vile mataifa ya BRICS – Afrika Kusini, India na China, mataifa ya Ulaya kama Italia, na mataifa yanayoitwa chui wa Asia kama Malaysia.

Ambapo Rwanda ni mfano mzuri wa kujifunza kwa mataifa mengine manne ya Afrika Mashariki, mwalimu bora zaidi kwa serikali, taasisi na jamii za eneo hilo ni kuiangalia hali halisi ya maisha ya watu wao namna inavyodhalilishwa kwa ufisadi.

Maana kama inavyosema Transparency International kwenye ripoti yake hiyo “ufisadi unatafsirika kwa mateso ya kibinaadamu, ambapo familia za kimasikini zinaelemezwa zigo la kulipa hongo kumuona daktari na kupata huduma ya maji safi. Inapelekea kufeli kwa upatikanaji wa hata huduma za msingi kabisa kwa wanaadamu kama vile chakula, elimu na afya. Inakokozoa uwezo wa mataifa kujijengea miundombinu imara, kwani viongozi mafisadi hutwaa fedha za miradi hiyo na kuweka mifukoni mwao.”

Na wapi pengine zaidi ya Afrika Mashariki ambako ukweli huo unaonekana katika sura zake zote halisi?

Mwandishi: Mohammed Khelef/DW Kiswahili
Mhariri: Oummilkheir Hamidou