Maonesho ya dunia ya Shanghai yafunguliwa rasmi | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.04.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Maonesho ya dunia ya Shanghai yafunguliwa rasmi

Zaidi ya viongozi 20 wa serikali na mataifa wamehudhuria ufunguzi rasmi leo Ijumaa wa maonyesho makubwa ya dunia mjini Shanghai kwa mwaka huu 2010.

default

Pichani linaonekana banda la maonesho mjini Shanghai litakalokuwa likitumiwa na mataifa ya Afrika katika maonesho hayo.

Zaidi ya viongozi 20 wa serikali na mataifa wamehudhuria ufunguzi rasmi leo Ijumaa wa maonyesho makubwa ya dunia mjini Shanghai kwa mwaka huu 2010.

Rais wa China, Hu Jintao, amezindua maoynesho hayo kwa fashifashi na tamasha la muziki katika sherehe zilizofana kabla ya maonyesho hayo kufungua milango yake kwa watu wa kawaida hapo kesho Jumamosi.

Katika hotuba yake ya ufunguzi , Hu ameahidi maonyesho ambayo yatakuwa ya mafanikio na ambayo hayatasahaulika. Viongozi kutoka mataifa kadha ya kigeni waliohudhuria sherehe hizo , ambazo zilianza saa nane mchana saa za huko China, huku kukiwa na ulinzi mkali, ni pamoja na rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, hadi kiongozi namba mbili wa Korea ya kaskazini, Kim Yong Nam. Taifa hilo la Korea ya kaskazini, ambalo linaungwa mkono na China, linahudhuria kwa mara ya kwanza katika maonyesho kama hayo.

China pia imetoa banda maalum kwa mataifa ya Afrika. Wenyeji wa maonesho hayo ya China wameahidi kuwa yatakuwa maonyesho ambayo yatahudhuriwa na watu wengi kuliko maonyesho yoyote kama hayo ya dunia kwa kuhudhuriwa na zaidi ya watu milioni 70, wengi wao wakiwa ni Wachina, ambao wanatarajiwa kuhudhuria katika maonyesho hayo yatakayodumu kwa muda wa miezi sita.

Kiasi cha nchi 200 pamoja na mashirika 50 yamejenga mabanda yao ya maonesho katika eneo hilo lenye ukubwa wa kilometa 5 za mraba ufukweni mwa mto Huangpu. Watu watakaotembelea maonyesho hayo wanatarajia kupanga milolongo mirefu kuweza kuingia ndani ya uwanja wa maonyesho.

Maonyesho ya mwaka huu yanalenga katika changamoto za kupanuka kwa miji chini ya kauli mbiu , 'miji bora, maisha bora'. Mji wa Shanghai, wenye wakaazi milioni 18, ni mmoja kati ya miji kumi mikubwa ulimwenguni. Maonyesho ya dunia, ambayo ikifahamika hapo kabla kama maonesho ya ulimwengu, yamekuwa yakifanyika mara mbili ama tatu katika muongo mmoja tangu yalipofanyika kwanza mwaka 1851 katika eneo la Hyde Park mjini London.

Wakati mabanda yakigharimu mamia ya mamilioni ya dola, waoneshaji bidhaa wamekuwa wakitaka kupata faida kwa kushawishi utalii pamoja na aina nyingine za uwekezaji. Wadadisi wanakadiria kuwa maonyesho ya Shanghai yamegharimu dola bilioni 50 kuyaendesha. Naibu wa mkurugenzi wa ofisi inayotayarisha maonesho ya Shanghai Huang Jianzhi amesema kuwa ,kwa maonyesho tu huwezi mtu kutengeneza faida, hilo tumelifanyia kazi. Ndio sababu naweza kusema kuwa hatuwezi kupata hasara. Pamoja na hayo tutachukua sehemu ya gharama. Kwasababu itabidi wakaazi wa mji wa Shanghai wabebe gharama hizi kupitia soko la nyumba ambalo litapamba kwa haraka na itabidi kuzuwia hali hiyo. Hadi sasa sioni tatizo.

Maonyesho hayo yalikumbana na matatizo kadha magumu wakati wa ufunguzi wa majaribio wiki moja kabla ya ufunguzi rasmi kwa kuwapo makundi makubwa ya watu yaliyojikusanya katika maeneo ya upekuzi kwa ajili ya usalama na mabanda yenyewe.

Watayarishaji wanasisitiza kuwa matatizo yametatuliwa katika muda muafaka kabla ya uzinduzi.

Mara milango itakapofunguliwa rasmi kwa ajili ya watu wote kuyaona maonyesho hayo, kesho Jumamosi, nchi zinazoshiriki zitawania kila moja kumshinda mwezie katika kuonesha kile wanachotaka kuionyesha dunia, mtazamo ukitiliwa katika soko la China lenye watu bilioni 1.3.

Denmark imejitokeza kwa kuleta sanamu maarufu la nguva la mji wa Copenhagen kwa mara ya kwanza, Ufaransa imeleta picha za kuchora pamoja na picha za kuchonga za Rodin, wakati Italia inaonyesha kazi za bingwa wa kipindi cha mwamko cha sanaa. Caravaggio. India imewaleta nyota wa filamu kutoka nchini humo na banda la Canada litakuwa na hisia za kufikirika za sarakasi mamboleo za kundi la Cirque du Soleil.

Mwandishi : Sekione Kitojo / AFPE

Mhariri : Othman Miraj.

 • Tarehe 30.04.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NBO2
 • Tarehe 30.04.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NBO2
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com