Majeshi ya Muungano yauwa Wataliban 136 katika mapambano | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Majeshi ya Muungano yauwa Wataliban 136 katika mapambano

Vikosi vya muungano vinavyoongozwa na Marekani vimesema leo hii kwamba vimewauwa wapiganaji 136 wa Taliban katika mapambano ya siku kadhaa katika bonde lilioko mbali nchini Afghanistan lakini wenyeji wa maeneo yaliofanyika mapambano hayo wanasisitiza kwamba raia walikuwa ni miongoni mwa watu waliopoteza maisha yao.

Majeshi ya Marekani na Canada yakipiga darubini mapango walikojificha wapiganaji wa Taliban.

Majeshi ya Marekani na Canada yakipiga darubini mapango walikojificha wapiganaji wa Taliban.

Polisi inasema zaidi ya polisi 300 wamepelekwa kwenye Bonde la Zerkoh lilioko katika jimbo la Herat kudhibiti maandamano ya wenyeji wa eneo hilo kupinga vifo vya watu hao ambapo waandamanaji wamesikika wakipiga mayowe ya kifo kwa Marekani.

Mapema majeshi ya muungano yamesema kwamba Vikosi Maalum vya Marekani vikiandamana na polisi na wanajeshi wengine wa muungano waliyashambulia maeneo ya Taliban katika bonde hilo hapo jana.

Taarifa yao imesema kwamba wanajeshi hao walitumia mizinga,silaha ndogo ndogo na maroketi na wakati msaada wa kuimarisha mashambulizi hayo ulipowasili ndege za majeshi ya muungano zilidondosha mabomu kwenye sehemu kadhaa zilizotambuliwa kuwa za maadui.

Taarifa imesema ndege za mashambulizi zimeuwa wapiganaji 26 katika pande zote mbili za bonde hilo.Jumla ya maeneo saba ya maadui yaliteketezwa na wapiganaji 87 wa Taliban waliuwawa wakati wa mapambano yaliodumu kwa masaa 14.

Siku mbili kabla wapiganaji zaidi ya 70 walishambulia Kikosi Maalum cha Marekani na kikosi cha polisi wa Afghanistan wakati wakiwa kwenye doria ya usiku katika eneo hilo.

Vikosi vya usalama vilijibu mapigo kwa mashambulizi ya ardhini na angani na kuuwa Wataliban 49 askari mmoja wa Marekani pia ameuwawa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya majeshi ya mmungano kila tahadhari ilichukuliwa kuzuwiya majeruhi kwa raia wasiokuwa na hatia wa Afghanistan wakati wa mapambano hayo mawili na kwamba hakuna majeruhi ya raia yaliorepotiwa.

Lakini wananchi wenyeji wa eneo hilo la bonde ambalo liko kama kilomita 150 kusini mwa mji wa magharibi wa Herat wanasema raia ni miongoni mwa watu waliopoteza maisha yao.

Mmojawapo ya waandamanaji walioandamana kupinga vifo hivyo ameliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya simu watoto pia wameuwawa kuwa watu waliowauwa sio Wataliban ni raia kwamba wamewauwa raia wakiwemo watoto. Amesema hawawataki Wamarekani kwenye eneo lao.

Kumekuwepo na kesi kadhaa za kuuwawa kwa raia katika hatua za kijeshi dhidi ya uasi unaojaribu kuiangusha serikali ya Afghanistan inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi.

Hata hivyo maafisa wa serikali wanasema mara nyengine madai hayo yanakuwa ya uongo na yanakusudia kujenga chuki dhidi ya maelfu ya wanajeshi wa kigeni walioko nchini humo.

Majeshi ya muungano yanasema yanajaribu kupunguza uharibifu wa ziada lakini maafa hutokea wakati wanamgambo wanaposhambulia kutoka kwenye majengo ya makaazi ya raia.

Takriban umwagaji damu wote unaohusishwa na uasi ulioanzishwa baada ya kupinduliwa kwa Taliban miaka mitano iliopita umekuwa kusini na kusini mashariki ya Afghanistan lakini mwaka huu kumeshuhudiwa mashambulizi kadhaa magharibi mwa nchi hiyo.

Uasi huo ulikuwa wa maafa makubwa kabisa mwaka jana ambapo zaidi ya watu 4,000 waliuwawa wengi wao wakiwa waasi.

Takriban watu 1,000 wamepoteza maisha yao mwaka huu kutokana na umwagaji damu huku pande zote mbili vikosi vya usalama na wanamgambo vikizidisha mashambulizi yao baada ya kutulia katika kipindi cha majira ya baridi.

 • Tarehe 30.04.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHFF
 • Tarehe 30.04.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHFF

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com