Majadiliano ya Mazingira Bonn | Masuala ya Jamii | DW | 03.08.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Majadiliano ya Mazingira Bonn

Baada ya serikali ya Marekani kutofanikiwa kupitisha sheria ya ulinzi wa mazingira kuna wasiwasi kuwa majadiliano ya Umoja wa Mataifa yanayofanywa Bonn,Ujerumani yatakabiliwa na vikwazo.

Baada ya kuwa na majadiliano kwa zaidi ya mwaka mmoja, serikali ya Rais wa Marekani Barack Obama wiki iliyopita, ilishindwa kupitisha sheria ya ulinzi wa mazingira katika Seneti yake. Hiyo bila shaka itaathiri duru mpya ya majadiliano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa yaliyofunguliwa siku ya Jumatatu mjini Bonn. Kwani sasa Obama hatoweza kutimiza malengo yaliyokubaliwa kwenye mkutano wa Copenhagen kupunguza gesi zinazochafua mazingira. Afisa wa shirika la Kijerumani lisilo la kiserikali "Germanwatch" Sven Harmeling anasema:

""Naamini kuwa Marekani, haitoweza kujiwajibisha kisheria kuhusu makubaliano ya kimataifa, ambayo Bunge la Marekani litaidhinisha."

Hata hivyo, Harmeling anaamini kuwa Obama ana njia nyingi zingine, kama vile kuweka mwongozo wa kitaifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa. Lakini, hatua kama hizo hazitokuwa na uzito kama vile sheria ya kitaifa ya ulinzi wa mazingira. Katika mkutano wa Copenhagen Obama aliahidi kuwa hadi mwaka 2020,viwango vya gesi zinazotoka kwenye viwanda na kuchafua mazingira vitapunguzwa kwa asilimia 17, kulinganishwa na vile viwango vya mwaka 2005. Lakini kulilinganishwa na viwango vya mwaka 1990, hiyo basi ni sawa na kupunguza asilimia 4 tu.

Sasa ni matumaini ya wanaharakati wengi kuwa jitahada za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa zitapata msukumo mpya, hasa kutoka Umoja wa Ulaya na China. Hata mkuu mpya wa masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa katika Umoja wa Mataifa, Christiana Figueres amesema, nchi zinazoinukia kiuchumi, hazikujiwajibisha kwa mikataba yo yote, hata kwa Itifaki ya Kyoto. Lakini nchi hizo zimetambua kuwa uwezo wa kushindana katika masoko ya kimataifa katika siku zijazo, unategemea teknolojia safi. Kwa hivyo tangu miaka kadhaa, zimeanza kuwekeza katika sekta hiyo. Kwa mfano, mwaka uliopita pekee, China iliwekeza dola bilioni 40 katika teknolojia inayosaidia kulinda mazingira. Ulaya iliwekeza bilioni 30. Kwa hivyo, Umoja wa Ulaya hauna budi kujitahidi zaidi kupata maafikiano ili mkutano utakaofanywa mwezi wa Desemba mjini Cancun Mexico uweze kufungua njia ya kupatikana makubaliano mapya ya Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa. Wajumbe wana mikutano miwili tu mingine kumaliza kazi hizo kabla ya mkutano wa Mexico.

Mwandishi:Jeppesen,Helle/ P.Martin

Mhariri:M.Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com