1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya Uingereza yasema Assange haendi Marekani

Bruce Amani
27 Machi 2024

Mahakama ya nchini Uingereza imetoa uamuzi kuwa muasisi wa tovuti ya kuvujisha nyaraka za siri wa Wikileaks Julian Assange hawezi kuhamishiwa Marekani kwa mashitaka ya ujasusi.

https://p.dw.com/p/4e9ok
Stella Assange, Mke wa Julian Assange
Stella Assange, mke wa Julian Assange alihudhuria kesi ya mahakama Uingereza ya mumewe kuhamishiwa MarekaniPicha: Leon Neal/Getty Images

Mahakama ya nchini Uingereza imetoa uamuzi kuwa muasisi wa tovuti ya kuvujisha nyaraka za siri wa Wikileaks Julian Assange hawezi kuhamishiwa Marekani kwa mashitaka ya ujasusi isipokuwa kama maafisa wa Marekani watatoa hakikisho kuwa hatokabiliwa na adhabu ya kifo.

Uamuzi huo umempa Assange ushindi wa sehemu katika mapambano yake ya muda mrefu ya kisheria kuhusu uchapishwaji wa nyaraka za siri za Marekani kwenye tovuti hiyo.

Soma pia:Bunge la Australia lataka muasisi wa WikiLeaks arejeshwe

Majaji wawili wa Mahakama ya Juu Victoria Sharp na Jeremy Johnson wamewapa maafisa wa Marekani wiki tatu kutoa hakikisho zaidi kuhusu kitakachomfanyikia Assange ambaye ni raia wa Australia.

Uamuzi huo una maana kuwa sakata hilo la kisheria, ambalo limedumu kwa zaidi ya muongo mmoja, litaendelea na Assange atabaki ndani ya Gereza la Belmarsh la London lenye ulinzi mkali, ambako amekaa kwa miaka mitano iliyopita.