1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUholanzi

ICJ kuamua juu ya mamlaka ya kusikiliza kesi dhidi ya Urusi

Saumu Mwasimba
29 Januari 2024

Mahakama ya juu zaidi ya Umoja wa Mataifa imesema itatoa uamuzi wake Ijumaa kuhusu ikiwa inayo mamlaka au la ya kusikiliza kesi iliyowasilishwa na Ukraine ikiituhumu Urusi kwa ukiukaji wa sheria ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/4bnmm
Majaji katika mahakama ya kimataifa ya haki ICJ
Majaji katika mahakama ya kimataifa ya haki ICJPicha: Piroschka van de Wouw/REUTERS

Ukraine imedai  Urusi ilitumia tuhuma za uwongo ikiisingizia kufanya  mauaji ya kimbari dhidi ya watu wanaozungumza Kirusi wanaoishi Ukraine, kama sababu ya kuivamia nchi hiyo mwaka 2022.

Urusi kwa upande wake ilikataa kufika mbele ya mahakama hiyo ya kimataifa ya Haki, ICJ mnamo mwaka 2022 na badala yake ikafungua kesi ya kupinga mamlaka ya mahakama hiyo.

Aidha siku ya Jumatano mahakama hiyo pia itatoa uamuzi wake katika kesi nyingine tofauti kuhusu mgogoro wa nchi hizo mbili, ambapo Ukraine inaitaka mahakama hiyo iiamrishe Urusi ilipe fidia kwa uhalifu na mashambulio iliyoyafanya dhidi ya jimbo la Crimea.

Ukraine ilifungua kesi mwaka 2017 ikiishtaki Urusi kwa madai ya kuzibagua baadhi ya jamii katika rasi ya Crimea baada ya kulinyakua eneo hilo.