Mada Kuu-Uhamiaji na Maendeleo ya Kiuchumi | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 06.08.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Mada Kuu-Uhamiaji na Maendeleo ya Kiuchumi

Ingawa Ujerumani imeikabidhi Ureno wadhifa wa urais wa Umoja wa Ulaya tangu katikati ya mwaka huu,bado yashghulikia matayarisho ya mkutano wa kilele wa Afrika na Ulaya utakaofanywa mwezi wa Desemba.

Waziri wa Nje wa Ujerumani,Frank-Walter Steinmeier(kushoto) akizungumza na Rais wa Ghana,John Kufour wakati wa ziara yake ya hivi karibuni nchini Ghana

Waziri wa Nje wa Ujerumani,Frank-Walter Steinmeier(kushoto) akizungumza na Rais wa Ghana,John Kufour wakati wa ziara yake ya hivi karibuni nchini Ghana

Mkutano wa aina hiyo haujapata kufanywa tangu miaka sita iliyopita.Sababu ni Zimbabwe,kwani kiongozi wa kidikteta wa nchi hiyo hakubaliwi na nchi za Ulaya kama mshirika katika majadiliano yao.Uingereza hasa inahisi kushiriki kwa Zimbabwe ni kizuizi kwa mkutano wa aina hiyo.Kwa upande mwingine,Waafrika wanaojiepusha kumkosoa dikteta Mugabe wanazuia kuingilia kati kwa vyo vyote.

Hata hivyo,kuna mengi ya kujadiliwa katika hali ya hivi sasa ya kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi na kujadiliwa mikataba mipya ya kiuchumi kati ya Ulaya na Afrika.

Ureno iliyoshika wadhifa wa urais katika Umoja wa Ulaya imeshaarifu kuwa uhamiaji na ushirikiano wa kiuchumi ni mada zinazopaswa kupewa kipaumbele kwenye mkutano ujao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani,Frank-Walter Steinmeier,ambae hivi karibuni alikuwa na ziara ya siku tatu nchini Nigeria na Ghana amesema, mtazamo wa mataifa ya Kiafrika ni sawa na ule wa nchi za Ulaya kwamba mada ya ushirikiano wa kiuchumi,ipewe kipaumbele kwani mada hiyo inafungamana na suala la uhamiaji.

Katika siku zijazo sera za nje za Ujerumani, zitashughulikia zaidi mada ya Afrika.Lakini kuna matatizo magumu ya kisiasa ambayo hutazamwa tofauti na pande zote mbili.

Ukuaji wa kiuchumi wa asilimia 5 au 6 katika nchi za Kiafrika unatokana na maliasili.Kwa mfano, Nigeria inayotegemea mauzo ya mafuta na gesi;au Angola inayoweza kuchomoza kwa ukuaji wa kiuchumi wa kama asilimia 25.Lakini,umma haunufaiki na utajiri huo.Hali ya umasikini ingali mbaya sana. Ni dhahiri kuwa hapo,kuna kasoro na hiyo pia ni mada muhimu kwa Ulaya na suala hilo huenda likazusha majadiliano makali kwenye mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika.

Kwa maoni ya waziri Steinmeier,ni muhimu kuhakikisha kuwa nchi za Kiafrika zenye utajiri wa maliasili,zina nafasi ya kuwa sehemu ya mfumuko wa kiuchumi na utajiri huo kweli, uwanufaishe wananchi na hivyo ndio kutapatikana jamii iliyo tulivu.

Kwa upande mwingine,waziri wa ulinzi wa Ghana,Albert Kann Dapaah,ambae nchi yake hivi sasa imeshika wadhifa wa urais katika Umoja wa Afrika alipoeleza fikra zake kuhusu mkutano wa kilele wa Ulaya na Afrika alisema,huu ni wakati kwa Ulaya na Afrika kukutana.Kwa maoni yake hiyo, ni hatua nzuri ya mwelekeo mwema.

Ulaya imeshasema kuwa mwishoni mwa mkutano huo wa kilele kutakuwepo mkakati wa pamoja wa Ulaya na Afrika.Ikiwa hilo kweli litatokea,haijulikani kwani bado kuna tatizo la Zimbabwe.Kwa hivi sasa wanadiplomasia wanajaribu kuifahamisha serikali ya Zimbabwe kuwa itakuwa bora kama haitoshiriki katika mkutano wa kilele.Ingawa Umoja wa Ulaya umeamua kuwa kushiriki kwa Zimbabwe kusiwe kizuizi,kuna baadhi ya nchi za Ulaya zilizosema, hazitohudhuria mkutano huo,ikiwa Zimbabwe itakuwepo.

Bila shaka ipo haja ya kufanywa mikutano ya kilele zaidi,kati ya Afrika na Ulaya,ili kuweza kujadili masuala muhimu yanayohusika na demokrasia,kupiga vita umasikini na kupata maendeleo kwa kila mmoja.Kwa hivyo,mkutano wa mwezi Desemba unaweza kuwa mwanzo wake.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com