1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron: China itumie ushawishi wake kusitisha vita Ukraine

6 Mei 2024

Rais wa Ufaransa Emanuel Macron na Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, wamemshinikiza rais Xi Jinping wa China kutumia ushawishi wa taifa lake kusitisha vita vya Urusi dhidi ya Ukraine

https://p.dw.com/p/4fYjN
 Xi Jinping Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amempokea leo Rais wa China Xi Jinping ambaye ameizuru nchi hiyo kwa ziara ya siku mbiliPicha: Yoan Valat/AP/picture alliance

Rais wa Ufaransa Emanuel Macron na Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya,Ursula von der Leyen, wamemshinikiza rais  Xi Jinping wa China ambaye yuko ziarani mjini Paris, Ufaransa kutumia ushawishi wa taifa lake kusitisha vita vya Urusi dhidi ya Ukraine. Mkutano huo wa kilele umejadili pia mahusiano ya kibiashara kati ya Ulaya na China. 

Ziara ya rais Xi ya siku mbili nchini Ufaransa ni ziara yake ya kwanza barani Ulaya tangu mwaka 2019 katika safari ambayo pia itampeleka  Serbia na Hungary ambako atafanya pia mazungumzo na viongozi wa mataifa hayo.

Soma zaidi. Macron afanya mazungumzo na Rais Xi Jinping mjini Paris

Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amesema mataifa ya ulaya yanafahamu kuwa China iko upande wa Urusi katika vita vyake dhidi ya Ukraine kwa kuipatia silaha na ndiyo maana inapaswa kutumia ushawishi wake kusitisha mzozo huo.

 China Xi Jinping  na  Emmanuel Macron
Rais Xi Jingping na mwenyeji wake Emmanuel MacronPicha: Ludovic Marin/AP/picture alliance

Akihutubia mkutano huo Mkuu huyo wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya amesema ´´tunakubali kwamba Ulaya na China zina maslahi ya pamoja katika kuleta  amani na usalama. Tunaitegemea China kutumia ushawishi wake wote kwa Urusi kumaliza vita vya Urusi dhidi ya Ukraine. Rais Xi amekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza kasi ya kutotumika kwa silaha za nyuklia za Urusi na nina imani kuwa Rais Xi ataendelea kufanya hivyo dhidi ya hali ya vitisho vinavyoendelea vya nyuklia vinavyofanywa na Urusi''.

Ursula: Ushirikiano wa kibiashara kati yetu upewe kipaumbele

Pamoja na mazungumzo hayo ya kiusalama lakini Rais Macron na Von der Leyen wote kwa pamoja wameonyesha kuwa suala la ushirikiano wa biashara kati ya Ulaya na China lazima lipewe kipaumbele.

Soma zaidi. Von der Leyen kupigia debe "ushindani sawa" na China

Kwa upande wake Rais Xi Jinping amesema kwa sasa dunia inakabiliwa na mabadiliko makubwa yenye misukosuko ndani yake na ushirikiano na kuaminiana baina ya China na Ulaya ndiyo ngao muhimu kwa sasa.

von der Leyen
Mkuu wa Kmaisheni ya Ulaya Ursula Von der leyen amemshinikiza rais Xi kutumia ushawishi wake kwa Urusi kusitisha vita byake dhidi ya UkrainePicha: Dimitar Dilkoff/AFP

"Dunia ya leo imeingia katika kipindi kipya cha misukosuko na mabadiliko. China na Ulaya kwa pamoja ni nguvu mbili muhimu duniani na zinapaswa kuzingatia msimamo wao wa ushirikiano, mazungumzo na ushirikiano, kuzidisha mawasiliano ya kimkakati, kuaminiana kimkakati, kuimarisha maelewano ya kimkakati, kukubaliana, kushirikiana na kukuza maendeleo imara na yenye afya ya uhusiano kati ya China na Ulaya."amesema Xi.

Soma zaidi. Rais Xi Jinping wa China aanza Jumapili ziara barani Ulaya

Hapo kesho Xi ataongozana na Macron kuitembelea milima ya Pyrenee ambayo alizoea kuitembelea alipokuwa kijana na baada ya hapo ataendelea na ziara yake katika mataifa ya Serbia na Hungary.

Tukumbushe kuwa hivi karibuni viongozi mbalimbali wa mataifa makubwa duniani waliizuru China akiwemo Kansela wa Ujerumani,Olaf Scholz na Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken na wote waliyagusia masuala ya mizozo inayoendelea duniani pamoja na ushirikiano wa kibiashara kati yao na China huku pia kukiwepo malalamiko ya mataifa ya Ulaya kwamba China inapelekea kutokuwepo kwa uwiano sawa katika soko la biashara la kimataifa.

Vyanzo: DPA na AFP
Mwandishi: Suleman Mwiru.