Maandamano ya Misri yaingia wiki ya tatu | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.02.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Maandamano ya Misri yaingia wiki ya tatu

Maandamano ya kumtaka Rais Hosni Mubarak wa Misri ajiuzulu yanaingia katika wiki yake ya tatu, huku waandamanaji wakishikilia madai yao na Mubarak akiendelea kuyapinga na jumuiya ya kimataifa ikiongeza shinikizo.

Maandamano dhidi ya Mubarak yaendelea

Maandamano dhidi ya Mubarak yaendelea

Ni siku ya 16. Maandamano yanaendelea. Upinzani dhidi ya Rais Hosni Mubarak unazidi kukua. Wanachama wa chama chake wanamkimbia na kujiunga na waandamanaji.

"Nilikuwa mwanachama wa chama tawala cha National Democratic. Sasa nimekiacha chama hiki kichafu ambacho watu wanakichukia." Anasema mwanamke mmoja, ambaye hivi sasa yupo katikati ya waandamanaji.

Rais Mubarak naye anazidi kuendelea kukaidi matakwa ya waandamanaji ya kuondoka madarakani, lakini ameamua kutumia mbinu ya kutoa kidole, kisha kiganja, kisha mkono. Haijulikani bado ni lini atakubali kusalimisha na kichwa chake kabisa.

Rais Mubarak azidi kulainika?

Rais Hosni Mubarak

Rais Hosni Mubarak

Mapema jana (8 Februari 2011), kupitia kwa Makamo wake Omar Suleiman, aliwapa waandamanaji kitu chengine, mbali ya vile kuongeza mishahara ya wafanyakazi wa serikali kwa asilimia 50, kuanzisha kamati za kuchunguza mashambulizi dhidi ya waandamanaji na kuahidi kutogombea tena hapo mwezi Septemba.

"Rais ameagiza kwamba hakutakuwa na mashtaka, mashambulizi wala kisasi dhidi ya waandamanaji wala haki yao ya kuwa na mawazo huru na kutoa maoni." Alisema Suleiman katika taarifa yake kwa taifa.

Umoja wa Mataifa waongeza shinikizo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon

Umoja wa Mataifa nao, kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Ban Ki-mmon, inaendelea na msimamo wake wa kutaka mabadiliko makubwa yanayodaiwa nchini Misri, ingawa, haimwambii Mubarak aondoke.

"Viongozi wa serikali lazima wasikilize kikamilifu matakwa halali ya watu, na kuwe na kipindi cha mpito haraka iwezekanavyo." Amesema Ki-moon.

Waandamanaji wameendelea kulalia na kuamkia uwanja wa Tahrir, ambapo sasa wamepageuza kama sehemu ya kufanyia ibada ya Hija.

Jana baadhi yao waliripotiwa kuelekea kwenye Bunge la nch hiyo, hatua ambayo huenda leo hii ikapata uungwaji mkono zaidi.

Mwanasheria mmoja, kijana wa miaka 35, Essam Magdi, ambaye amekuwa akilala chini ya vifaru vya wanajeshi vilivyozagaa kwenye uwanja wa Tahrir, alisikika akiapa kuwa hawatarudi nyuma.

"Hakutakuwa na maafikiano yoyote mpaka Mubarak aondoke. Akishaondoka yeye tu, tunaweza sasa kuzumngumzia masuala mengine." Amesema Magdi.

Marekani yajirudi?

Rais Hosni Mubarak na Rais Barack Obama

Rais Hosni Mubarak na Rais Barack Obama

Kwengineko ulimwenguni, Ikulu ya Marekani, ambayo ni rafiki mkubwa wa utawala wa Rais Mubarak, na ambayo kwa siku za karibuni, imekuwa ikilaumiwa kwa kigeugeu chake kwenye mgogoro huu, imeripotiwa kutafuta njia za kuweka sawa taswira yake.

Shirika la Habari la AP, limesema kuwa, maoni ya mjumbe maalum wa Rais Barack Obama kwa Rais Mubarak, Frank Wisner, kwamba ingelikuwa vyema Mubarak akabakia madarakani, kusimamia mchakato wa kuirejesha Misri kwenye demokrasia, yalimkera sana Rais Obama.

Huko nchini Ufaransa, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, François Fillon, amekiri kwamba sehemu fulani ya mapumziko yake ya mwezi Disemba mwaka jana, yalilipiwa na Rais Mubarak.

Tukio hili, likiwa ni la pili kwa mawaziri wa serikali ya Rais Nicolas Sarkouzy, limetafsiriwa na wakosoaji, kama ni mfano wa wanasiasa wa nchi za Magharibi, wanavyojifaidisha na watawala wa kidikteta katika Afrika na Arabuni.

Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Michel Alliot-Marie, alikiri kutumia ndege binafsi inayomilikiwa na mshirika wa karibu wa rais wa Tunisia aliyefurushwa madarakani, Zein El-Abidine Ben Ali.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFPE/DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com