1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leverkusen yatinga fainali Kombe la Shirikisho - DFB Pokal

4 Aprili 2024

Klabu ya soka ya Bayer Leverkusen iliyo kileleni mwa ligi kuu ya kandanda nchini Ujerumani Bundesliga, usiku wa kuamkia leo imefanya maajabu mengine kwa kutinga fainali ya kuwania Kombe la Shirikisho, DFB Pokal.

https://p.dw.com/p/4ePGS
Leverkusen | Bayer Leverkusen vs Fortuna Düsseldorf | DFB-Pokal
Mtanange wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho nchini Ujerumani kati ya Bayer Leverkusen na Fortuna Düsseldorf. Leverkusen iliichapa Düsseldorf bao 4-0 kwenye dimba la BayArena.Picha: Martin Meissner/AP Photo/picture alliance

Leverkusen imeendeleza ubabe wake kwenye kambumbu kwa kuicharaza Fortuna Dusseldorf bao 4-0 kwenye mchezo wa nusu fainali ya kombe la shirikisho uliopigwa kwenye dimba la BayArena mjini Leverkusen.

Ushindi huo wa Leverkusen unaisafishia njia zaidi klabu hiyokuelekea kuandika historia ya kuchukua makombe matatu msimu huu. Tayari wanapigiwa upatu wa kuwa mabingwa wa Bundesliga na pia wametinga robo fainali ya kupigania Europa Cup.

Kwenye kinyang´anyiro cha DFB Pokal, vijana hao wa kocha Xabi Alonso sasa watakutana na klabu ya Kaiserslautern kwa mchezo wa fainali utakaopigwa mnamo Mei 25. Kaiserslautern walijikatia tiketi ya kucheza fainali Jumanne wiki hii kwa kuichapa Saarbrucken bao 2-0.