1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Larijani: "Iran haiogopi vitisho vyako Trump"

10 Machi 2026

Mkuu wa usalama wa Iran Ali Larijani amemuonya Rais wa Marekani Donald Trump akisema Iran haiogopi vitisho vyake.

https://p.dw.com/p/5A7Vw
Mkuu wa ulinzi wa Iran, Ali Larijani
Mkuu wa ulinzi wa Iran, Ali LarijaniPicha: Bilal Hussein/AP Photo/picture alliance

Larijani ameyasema haya wakati ambapo Israel imeanza kufanya wimbi jipya la mashambulizi huko Tehran Jumanne huku kambi ya kijeshi inayotumiwa na vikosi vya Ujerumani huko Jordan ikishambuliwa na Iran.

Katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa X, mkuu wa usalama wa Iran Larijani amemwambia Trump awe makini baada ya rais huyo katika ujumbe ambao naye aliuandika kwenye mtandao wake wa Truth Social, kuitishia Iran kuwa itashambuliwa zaidi na Marekani iwapo itazuia meli za mafuta kupita katika njia ya Hormuz. Larijani amemjibu Trump, kwa kumwambia vitisho vyake ni maneno matupu.

Haya yanafanyika wakati ambapo jeshi la Israel limesemalimeshambulia maeneo kadhaa mjini Tehran leo ikiwemo jengo moja lililoko chini ya ardhi ambalo hutumiwa na Jeshi la Mapinduzi la Iran kwa ajili ya kufanyia majaribio makombora, lililoko katika "chuo kikuu cha kijeshi."

Shirika la habari la Ufaransa AFP halikuweza kuthibitisha mashambulizi hayo.

Kambi ya jeshi la Ujerumani yashambuliwa

Kwengineko mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel yameushambulia uwanja wa ndege kusini mwa Iran na kusababisha uharibifu wa sehemu ya uwanja huo pamoja na ndege kadhaa. Haya ni kulingana na vyombo vya habari vya Iran.

Waokoaji wakirekebisha jengo baada ya shambulizi la Iran mjini Tel Aviv
Waokoaji wakirekebisha jengo baada ya shambulizi la Iran mjini Tel AvivPicha: Gil Cohen Magen/Xinhua/IMAGO

Haijawa wazi uiwapo kuna kambi yoyote ya kijeshi karibu na uwanja huo, ingawa jana jeshi la israel lilisema kuwa lilifanya mashambulizi katika viwanja sita vya kijeshi nchini Iran ambapo ndege na njia za kurukia ndege zilishambuliwa pamoja na mifumo ya ulinzi.

Hayo yakijiri, kambi moja ya kijeshi nchini Jordan ambayo inatumiwa na jeshi la Ujerumani imeshambuliwa kwa makombora na Iran Jumanne. Kwa mujibu wa msemaji wakamandi ya operesheni ya jeshi la Ujerumani, Bundeswehr, sehemu iliyo na wanajeshi wa Ujerumani ya kambi ya al-Azraq ndiyo iliyoshambuliwa.

Amesema kuwa wanajeshi wa Ujerumani walioko katika kambi hiyo lakini wako salama katika maeneo yaliyo na ulinzi. Kulingana na takwimu za wizara ya ulinzi ya Ujerumani, zaidi ya wanajeshi 500 wa Ujerumani wamekita kambi huko Mashariki ya Kati ambapo karibu wanajeshi 200 wako Irak, Jordan na Lebanon.

Iran pia imeushambulia mji wa Tel Aviv leo kwani sauti za milipuko zimesikika mjini humo huku ving'ora vikisikika kuwaonya raia kukimbilia maeneo salama. Mifumo ya ulinzi wa angani ya Israel inaripotiwa kuzuia baadhi ya makombora muda mfupi baada ya jeshi la Israel kutoa tahadhari ya shambulizi.

Wakati huo huo, Qatar imesema kuwa inataka kuimarisha ushirika wake wa ulinzi na Marekani kufuatia mashambulizi ya Iran. Kulingana na msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Qatar Majed Al Ansari, ushirikiano ulioko sasa kati ya Qatar, Marekani na washirika wake wa Ulaya hautiliwi shaka ila unastahili tu kuimarishwa.

"Kulenga miundo mbinu muhimu iwe ni mifumo ya kusafisha maji, matangi ya maji, hifadhi za chakula, hifadhi za madawa, miundo mbinu yoyote ambayo inasaidia maisha ya watu, ni hatari kubwa kwa watu wa eneo hili na ni jambo linalostahili kusitishwa mara moja," alisema Ansari.

Tamko hilo la Qatar linakuja wakati ambapo Shirika la Afya Duniani WHO limeonya kuwa "mvua nyeusi" inayonyesha nchini Iran baada ya hifadhi za mafuta kushambuliwa na Israel, inaweza kusababisha matatizo ya kupumua.

"Mvua nyeusi" kuleta matatizo ya kupumua

WHO inasema impokea ripoti za mvua iliyochanganyika na mafuta wiki hii kufuatia shambulizi hilo lililosababisha anga za mji wa Tehran kufunikwa na moshi mweusi.

Wakati huo huo wachezaji watano wa timu ya kandanda ya wanawake ya Iran wamepewa hifadhi nchini Australia walikokuwa wamekwenda kushiriki mashindano ya Kombe la bara Asia. Wachezaji hao walikuwa wanatafuta ulinzi baada ya kuitwa "wasaliti" nchini Iran kwa kukataa kuimba wimbo wa taifa.

Wachezaji wa timu ya taifa ya kandanda ya wanawake ya Iran wakishiriki mashindano ya Bara Asia huko Australia
Wachezaji wa timu ya taifa ya kandanda ya wanawake ya Iran wakishiriki mashindano ya Bara Asia huko AustraliaPicha: Str/AFP

Rais wa Marekani Donald Trump ni miongoni mwa waliokuwa wametoa mwito kwa Australia kuwapa hifadhi wachezaji hao, akisema wangekuwa kwenye hatari kubwa iwapo wangerudi Iran.

Wachezaji watano akiwemo nahodha Zahra Ghanbari walikimbia kutoka kwenye hoteli ya timu hiyo usiku na kujificha kwa maafisa wa Australia.

Vyanzo: AFP/DPA/Reuters