Kutana na Mwalimu Julius Nyerere | Media Center | DW | 25.07.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Media Center

Kutana na Mwalimu Julius Nyerere

Kutana na Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa waziri mkuu wa Tanganyika, baadaye Tanzania na hatimaye Rais wa kwanza wa Tanzania. Tizama maono yake, ambayo yalikuwa ni pamoja na kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki.

Tazama vidio 01:26
Sasa moja kwa moja
dakika (0)

Mwanachama dhahiri wa vuguvugu la muungano wa Afrika, Nyerere aliiongoza Tanganyika kupata uhuru kutoka Uingereza na baadae akaiunganisha na Visiwa vya Zanzibar na kuunda Tanzania ya leo. Licha ya mapungufu yake, sera yake ya Ujamaa inasifiwa kwa kuipa Tanzania utambulisho wa kitaifa.

Nyerere aliishi wapi?

Alizaliwa 1922 katika kijiji cha Butiama, wilaya ya Musoma, mkoani Mara katika iliyokuwa Tanganyika ambayo sasa ni Tanzania. Alisomea ualimu katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda na baadae alisomea Uchumi na Historia katika Chuo Kikuu cha Edinburgh, Uskochi. Alifariki 1999 mjini London, Uingereza.

Alijulikana kwa kitu gani?

Alijulikana zaidi kwa jina lake la "mwalimu". Nyerere kwa hakika alisomesha Baiolojia na Kiingereza kwa miaka mitatu kabla ya kuiongoza Tanganyika katika kupata uhuru na baadaye kuwa rais wa kwanza wa Tanzania.

Alipenda sana kuiona Afrika inaungana na kuwa moja. Lakini alipingana na Kwame Nkrumah wa Ghana katika suala hilo. Nyerere alitaka hatua ya kwanza iwe kuungana kwa nchi za Afrika Mashariki, wakati Nkrumah akigombania kuungana kwa nchi zote za Afrika kwa wakati mmoja. Kwa kushirikiana hata hivyo, waliunda Umoja wa nchi huru za Afrika, OAU. Nyerere aliwakaribisha wapiganaji wa uhuru. Baaada ya kupata uhuru wa nchi yake, aliwakaribisha na kuwaunga mkono waasi waliokuwa wakizipinga serikali za Msumbiji, Afrika Kusini, Namibia na nyinginezo.

Julius Nyerere, 1. Präsident Tansanias feiert Unabhängigkeit seines Landes (Comic Republic)

uliua Nyerere akishangilia uhuru wa Tanganyika mwaka 1961

Julius Nyerere alikuwa anajulikana sana kwa kitu gani kingine?

Mwalimu Nyerere alitafsiri katika lugha ya Kiswahili vitabu vya mwandishi gwiji wa Kiingereza, William Shakespeare.

Nyerere alikuwa mkaidi kwa kiasi gani?

Katika kipindi cha Vita Baridi, Nyerere hakuegemea upande wowote. Wakati Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani iliiomba Tanzania kuachana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani kulingana na Kanuni zake za Hallstein lakini Nyerere alikataa, akiwa tayari hata kupoteza misaada ya kimaendeleo iliyokuwa ikitoka Ujerumani, alisisitiza juu ya umuhimu wa uhuru wa Tanzania. Alisema nchi yake "haitakubali msaada kwa masharti" - na hatimaye aliwashinda. Nchi yake iliimarisha uhusiano wa kidiplomasia na Ujerumani zote mbili za wakati huo.

Julius Nyerere alikosolewa kwa mambo gani?

Alikosolewa kwa kumkandamiza yeyote anayetoa maoni ya kumpinga, kuwatenga wapiganaji wengine wa uhuru , na kuchukua sifa zote peke yake. Anatajwa pia kwa kupinga kuwepo ushawishi wa viongozi wa Kiislamu nchini Tanzania. Muhimu zaidi, sera yake ya Ujamaa wa Afrika haikufanikiwa kubadilisha hali ya uchumi wa Tanzania. Kutokana na hilo, Nyerere aliachia madaraka 1985 kusafisha njia kwa marekebisho ya miundo ya kiuchumi.

DW Videostill Projekt African Roots | Julius Nyerere, Tansania (Comic Republic)

Jukius Nyerere, rais wa kwanza wa Tanzania

Sijawahi kusikia juu ya Ujamaa. Unamaanisha nini hasa?

Kutokana na kwamba alitoka katika familia kubwa, na mfuasi ya jumuiya ya watu wenye kuunga mkono falsafa ya ujamaa nchini Uingereza (British Fabian Society), Nyerere alianzisha mfumo wa Ujamaa wa Afrika uliojaribu kujumuisha mfumo wa maisha wa Kiafrika wa kuishi kwa pamoja. Alijadiliana na Jomo Kenyatta, na kuna wakati alikuwa tayari kumpa nafasi Kenyatta kuwa kiongozi wa Afrika Mashariki yote. Alikuwa tayari hata kuusogeza mbele uhuru wa Tanganyika, na kuzingoza nchi nyingine tatu za Afrika Mashariki kupata uhuru wao kwa matumaini ya kuungana pamoja baadae. Viongozi wengine wa nchi hizo za Afrika Mashariki walimuendea kinyume lakini hilo halikumrudisha nyuma Nyerere. Alielekeza juhudi zake katika kuyaunganisha pamoja makabila mbalimbali ya Tanzania kwa mfano moja ya mbinu alizozitumia ni kuhakikisha Kiswahili kinazungumzwa na wote kama lugha ya taifa.

Nyerere alikuwa na misemo gani maarufu?
"Uhuru na kazi"
"Hakuna taifa lenye haki ya kufanya maamuzi juu ya taifa lingine; wala hakuna mtu mwenye haki ya kumfanyia maamuzi mtu mwengine"
"Umoja hautatufanya tuwe matajiri, lakini itaifanya vigumu kwa Afrika na Waafrika kupuuzwa na kufadhaishwa."
"Elimu sio njia ya kuepukana na umaskini, ni nia ya kuapambana nao."
"Ili kupata maendeleo ya kweli, watu lazima wahusishwe."

James Muhando, Hawa Bihoga na Gwendolin Hilse wamechangia kuandika makala hii. Ni sehemu ya makala maalum za  mfululizo wa "Asili ya Afrika", ushirikiano kati ya shirika la DW na taasisi ya Gerda Henkel.

Tafsiri: Yusra Buwayhid
Mhariri: Grace Patricia Kabogo