1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya maoni ya Papandreou yawagawa wengi

2 Novemba 2011

Baraza la Mawaziri la Waziri Mkuu George Papandreou limekubali pendekezo la kura ya maoni juu ya mkopo wa euro bilioni 130, huku Waziri Mkuu huyo akielekea kukutana na viongozi wakuu wa kanda ya euro kuwashawishi.

https://p.dw.com/p/133Xy
Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou.
Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou.Picha: dapd

Haikuwa kazi rahisi kupata uungwaji mkono wa ndani ya nchi yake, na imeshafahamika kuwa itakuwa vigumu zaidi kuungwa mkono nje ya nchi yake.

Baadhi ya wabunge kutoka upinzani na hata wa chama chake mwenyewe, wamemtaka Waziri Mkuu Papandreou ajiuzulu, wakimtuhumu kuutia rehani uwanachama wa Ugiriki kwenye mataifa yanayotumia sarafu ya euro.

"Kwa kutafuta kuiokoa nafsi yake, Papandreou amekuja na kizungumkuti hiki cha ghilba, ambacho kitauweka hatarini mustakabali wetu na nafasi yetu kwenye bara la Ulaya." Amesema Andonis Samaras wa chama cha upinzani cha kihafidhina.

Utetezi wa Papandreou kwamba uamuzi huu wa kura ya maoni ni kuipa demokrasia nafasi yake ili umma wa Ugiriki uamue juu ya kile unachotaka kwa mustakabali wa maisha yao, haujawaingia wengi.

Baada ya kuungwa mkono na baraza lake mwenyewe la mawaziri, sasa Papandreou anakabiliwa na mtihani mgumu mbele ya Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa, viongozi ambao walijitolea 'pawa na miko' kuhakikisha kuwa Ugiriki inapatiwa msaada wa kujiokoa isifilisike. Viongozi hao wamemwita Papandreou leo (02.11.20119 kabla ya mkutano wa mataifa ya G20 mjini Cannes, Ufaransa.

Viongozi wa dunia wafadhaishwa

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani (kushoto) na Rais Nikolas Sarkozy wa Ufaransa.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani (kushoto) na Rais Nikolas Sarkozy wa Ufaransa.Picha: picture alliance/dpa

Mapema Rais Sarkozy alikuwa amesema katika hotuba yake kwenye televisheni kuwa tangazo la Waziri Mkuu Papandreou "liliishangaza Ulaya nzima".

Inatarajiwa kwamba Rais Sarkozy atakuwa mkali zaidi kuliko alivyokuwa kwenye mkutano wa mwisho wa viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya wa wiki iliyopita, ambapo alimkaripia Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, kwa kujiingiza kwenye mambo ya sarafu ya euro. Uingereza si mwanachama wa sarafu ya euro, ingawa ni mjumbe muhimu wa Umoja wa Ulaya.

Mara baada ya tangazo la Papandreou, Kansela Merkel na Rais Sarkozy walikutana kwa dharura hapo jana, ingawa hawakutoa kauli yoyote hadharani baada ya mkutano wao.

Waziri wa Fedha wa Japan, Jun Azumi, amesema hivi leo kuwa "kila mtu ametishwa na uamuzi huu" wa Papandreou, huku wizara ya Mambo ya Nje ya China ikitoa kauli inayoashiria kushitushwa na uamuzi ho.

"China imepokea taarifa za kura ya maoni ya Ugiriki. Lakini tunatarajia kuwa Ulaya itaendelea kubakia kwenye mpango uliokubaliwa wiki iliyopita wa kuutatua mgogoro wa madeni yake." Amesema msemaji wa wizara hiyo, Hong Lei, hivi leo

China inatarajiwa kuchukuwa dhima kubwa

Mkuu wa Mfuko wa Uokozi wa Sarafu ya Euro, Klaus Regling, akizungumzia juu ya haja ya China kuchangia utatuzi wa mgogoro wa euro.
Mkuu wa Mfuko wa Uokozi wa Sarafu ya Euro, Klaus Regling, akizungumzia juu ya haja ya China kuchangia utatuzi wa mgogoro wa euro.Picha: dapd

China, ikiwa moja ya mataifa yanayoinukia chini ya umoja wa BRICS, inashiriki mkutano wa mataifa ya G20 unaoanza hapo kesho nchini Ufaransa, ambapo suala la madeni ya kanda ya euro ni miongoni mwa ajenda kuu.

Tayari Ulaya imeshaiomba China kuusaidia kifedha mfuko wake wa uokozi, huku taifa hilo la Mashariki ya Mbali likiwa tayari mshikiliaji mkubwa wa deni la Ulaya na likiwa limesharejelea mara kadhaa msimamo wake wa kuitaka "Ulaya irekebishe mfumo wake wa kifedha".

Kama kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa, msemaji wa serikali ya Ugiriki, Ilias Mosialos, amesema kura hii ya maoni itafanyika mara tu baada ya mambo ya msingi kuhusiana na msaada wa fedha kutoka Umoja wa Ulaya na Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) kurekebishwa.

Hii inamaanisha kuwa ni aidha mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu au mwanzoni mwa mwezi Januari, mwakani.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AFP
Mhariri: Othman Miraji