1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kupelekwa Radovan Karadzic mbele ya Mahakama ya The Hague

Othman, Miraji30 Julai 2008

Radovan Karadzic akabidhiwa kwa Mahakama ya Kivita ya The Hague

https://p.dw.com/p/EnP8
Radovan Karadzic, kiongozi wa zamani wa Wa-Serbia wa Bosnia, baada ya kukamatwa mjini Belgrade.Picha: AP

Ilikua habari nzuri kwa Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ya The Hague. Kiongozi wa zamani wa Wa-Serbia wa Bosnia, Radovan Karadzic, jana usiku alikabidhiwa kwa mahakama hiyo. Sasa itabidi ajielezee juu ya mashtaka anayokabiliana nayo juu ya mauaji ya kiholela ya Waislamu katika Vita vya kienyeji vya Bosnia.

Naam, matarajio yamekamilika. Mhalifu wa kivita anayeshukiwa na aliyekuwa anatafutwa kwa udi na uvumba sasa amewasili Uholanzi. Wale mawakili wake waliofikiri wataweza kuchelewesha kupelekwa kwake huko The Hague wameambulia patupu. Mtuhumiwa huyo, aliyejipagaza jina la Daktari Dabic na kujifaragua na kujipatia burudani katika maeneo ya fukwe za Bahari ya Adriatik, katika siku za mbele atasikia tu sauti za mawimbi ya bahari. Mahala atakapoishi sasa ni huko Uholanzi katika Bahari ya Kaskazini, masafa yanayochukuwa dakika tano kwa gari kutoka jengo la Mahakama ya Umoja wa Mataifa inayowashughulikia wahalifu wa kivita.

Kumekuweko washtakiwa waliopelekwa mbele ya mahakama hiyo na ikabidi ichukuwe miaka hadi kesi zao zilipomalizika. Lakini mara hii waendeshaji mashtaka na mahakimu wataiharakisha kesi ya Radovan Karadzic. Mwendeshaji mashtaka ameshakusanya ushahidi wa kutosha kuweza kumtia hatiani kiongozi huyo wa zamani wa wa-Serbia wa Bosnia kwa mashtaka ya mauaji ya kiholela na vitendo vingine vya uhalifu. Mwedeshaji mkuu wa mashtaka, Serge Brammertz, na wasaidizi wake wanaweza kuchukuwa ushahidi wa kesi za zamani zilizosikilizwa katika mahakama hiyo. Imeshahakikishwa kwamba mauaji ya Srebrenica yalikuwa ya kimbari. Kwa kushiriki katika mauaji hayo, jenerali wa zamani wa Wa-Serbia wa Bosnia, Krstic, hivi sasa anatumikia kifungo cha miaka 35 gerezani.

Hakuna ubishi. Mtuhumiwa huyu wa sasa aliyekuwa anatafutwa kwa udi na uvumba yuko katika hatari ya kupewa hukumu ya kifungo cha maisha gerezani.

Lakini mshtakiwa huyu ana nafasi ya kuirefusha kesi hiyo na kuutumia vibaya ukumbi wa mahakama kama jukwaa la kisiasa, kama vile alivofanya Slobodan Milosevic aliyekufa kizuizini. Na kama alivofanya rais huyo wa zamani wa Yogoslavia, Radovan Karadzic pia atajitetea mwenyewe binafsi mahakamani, akisaidiwa na washauri kadhaa. Kwa hivyo yaonesha kutakuweko pata shika mahakamani. Kwa hivyo itakuwa vizuri kwa waendeshaji mashtaka wakadurusu upya mashtaka.

Bibi Carla del Ponte, mwendeshaji mashtaka aliyekuwa na bashasha lakini machachari kama alivyo wa sasa, yaani Bwana Brammertz, hati zake za mashtaka zilikuwa nyingi mno, hivyo kusababisha vikao vingi. Katika mkasa wa Slobodan Milosevic ilichukua muda mrefu hata mshtakiwa mwenyewe akafa kabla ya kuhukumiwa.

Bila yashaka, ni jambo linalofaa kwamba mtuhumiwa lazima ajibu kuhusu yale yote alioyatenda, lakini muhimu zaidi ni kwamba wahalifu wa Vita vya Yogoslavia angalau wanahukumiwa. Carla Del Ponte mara kadhaa ameyasambaza mambo kwa vile alitaka kuisahihisha historia na kuweka mfano. Mrithi sake, naamini, hatotaka hayo.

Serge Brammertz ni mtu mtulivu, aliye makini, lakini mwanasheria aliye mkakamavu. Huenda, kutokana na umahiri wake wa kidiplomasia ndio maana wakuu wa Serbia wakamkamata Radovan Karadzic. Mwanasheria huyo wa Kibelgiji aliweza faraghani kuungwa mkono na watu, watu ambao walikataa kushirikiana kabisa na Carla del Ponte.

Kwa hivyo, Umoja wa Mataifa unabidi kwa haraka uweke mambo wazi na urefushe majukumu ya mahakama hiyo ya The Hague, kwani kesi zote zilioko huko The Hague zinatakiwa zimalizike kusikilizwa ifikapo mwisho wa mwaka huu. Hilo halitawezekana. Sasa uamuzi unatarajiwa kutolewa, na licha ya malalamiko yote, mahakama hiyo imedhirisha haki ya kuweko kwake. Historia ya mahakama hiyo ni historia ya mafanikio.