Kumbukumbu ya mashumbilizi ya Mumbai
26 Novemba 2009Ni shambulizi lililozidisha zaidi mgogoro kati ya majirani wawili Pakistan na India- hasa ilipobainika kundi linaloitwa Lashkar e Taiba lenye makao yake Pakistan ndilo lililopanga uvamizi mjini Mumbai.
Na huku India leo, ikikumbuka- wanaendelea kuiwekea mbinyo serikali ya Pakistan kukabiliana na makundi yenye siasa kali humo, kwa kile wengi wanasema Pakistan imeregea katika kuangamiza vitisho vya makundi hayo.
Mtaalamu wa maswala ya usalama kutoka India, Waslekar Sundeep anasema
'' Utawala wa Pakistan kwa muda mrefu umekuwa ukiuunga mkono kwa siri ukishirikiana makundi ya kigaidi nchini humo. Na pia wana maslahi yao- na maslahi yao ni kujenga sura ya wasiwasi. Kwa sababu ugaidi kwa ujumla huwa ni kuzusha machafuko.''
Polisi nchini India wanashika doria katika mji wote wa Mumbai, huku wakionyesha zana zao za kisasa- ishara kwamba wako imara kwa lolote. Wabunge, na wachezaji cricket pia walijumuika na raia wengine nchini India kuweka mashada ya maua na kujumuika katika maombi kuwakumbuka watu 166 waliouawa katika shambulizi hilo.
Mishumaa iliwashwa katika Sinagogi moja ya Mumbai. Viongozi wa kidini, wanadiplomasia wa kimataifa waliungana na raia wa India, katika makumbusho hayo, wakitoa mwito wao amani na umoja katika kupigana na kuangamiza makundi ya kigaidi kote duniani.
Akiwa ziarani nchini Marekani, Waziri mkuu wa India Manmohan Singh aliitolea changamoto serikali ya Pakistan kufanya kila juhudi kuonyesha mkono wake wa sheria una nguvu, dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya kigaidi nchini humo, ambao bado huru kutekeleza mashambulizi katika eneo hilo.
Mwaka mmoja uliopita magaidi kumi waliuvamia mji wa Mumbai, katika shambulizi lililoitikisa nchi hiyo na kuushtua ulimwengu mzima. Ulimwengu mzima ulibakia mdomo wazi, pale picha za shambulizi hilo lililodumu kwa siku tatu, zilipeperushwa moja kwa moja katika televisheni kote duniani.
Kati ya washambulizi wote kumi ni mmoja tu ndiye aliyebaki hai, raia wa Pakistan ambaye tayari ameshtakiwa kwa mauaji. Jana mahakama ya kupambana na ugaidi nchini Pakistan iliwafungulia mashtaka watu sita kwa kuhusika na mashambulizi ya Mumbai. Wote lakini walikanusha mashtaka hayo.
Mwandishi: Munira Muhammad/ AFPE:
Mhariri: Abdul-Rahman