1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongamano la GMF lafunguliwa Bonn

Mohammed Khelef
20 Juni 2022

Kongamano la 15 la vyombo vya habari ulimwenguni limeanza mjini Bonn ikiwa ni mara ya kwanza kwa washiriki kukusanyika pamoja tangu janga la virusi vya korona lianze ulimwenguni mwishoni mwa mwaka 2019.

https://p.dw.com/p/4CxHC
GMF 2022
Picha: Ronka Oberhammer/DW

Kundi la STEGREIF lilitumbuiza kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa mjini Bonn mapema siku ya Jumatatu (Juni 20) kwa ajili ya kuwaweka sawa washiriki wa kongamano hilo la siku mbili ambalo maudhui yake makuu ni "Kuijenga kesho kwa kuanzia na leo."

Kongamano hilo lilifunguliwa na Mkurugenzi Mkuu wa DW, Peter Limbourg, ambaye kwenye hotuba yake aligusia ugumu wa kazi ya uandishi wa habari katika zama hizi za janga la UVIKO-19 na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, akisema, hata hivyo, lazima waandishi wa habari wasimame imara mbele ya majaribu hayo.

Washiriki zaidi ya 2,000 wakongamanohili walielezwa pia jinsi ukweli ulivyogeuka kuwa adui mkubwa mbele ya wenye mamlaka na makundi yenye nguvu ya kijamii, hali iliyomfanya mshindi wa mwaka 2021 wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Maria Ressa, kutoka Ufilipino kuishi kwa mashaka sehemu kubwa ya maisha yake ya kikazi.

Ukweli ndio msingi wa kuaminiwa

GMF 2022 | Peter Limbourg und Maria Ressa
Mkurugenzi Mkuu wa DW, Peter Limbourg (kushoto), akiwa na Maria Ressa, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa mwaka 2021 mjini Bonn.Picha: Ronka Oberhammer/DW

Kwenye kongamano la leo, Maria Ressa alipewa nafasi ya kutoa hotuba kuu ya mjadala, chini ya kichwa cha habari: "Je, uko tayari kujitolea kwa kiasi gani kwa ajili ya kusimamisha ukweli?", ambapo alisema kwamba ni lazima waandishi wawe na taarifa za kutosha ndipo wapate ukweli, ambao nao unajenga kuaminiwa na umma.

Wazungumzaji wengine kwenye siku hii ya kwanza ya kongamano hili la siku mbili, ambalo linahudhuriwa na washiriki kutoka mataifa zaidi ya 100 duniani, walikuwa ni Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani, Annalena Bearbock, Waziri Mkuu wa Jimbo la Northrhine Westphalia unakofanyika mkutano huu, Hendrick Wüst, na Claudia Roth, waziri mwenye dhamana ya utamaduni na vyombo vya habari katika serikali kuu ya shirikisho la Ujerumani.

Zaidi ya mada na warsha 40 zitaendeshwa kwenye kongamano hili la siku mbili, msisitizo ukiwekwa kwenye namna ambavyo taaluma ya uandishi wa habari inavyoweza kukabiliana na majaribu ya sasa katika ulimwengu uliojaa njia nyepesi na rahisi za kuwasiliana lakini zisizo za uhakika wala usimamizi.

Miongoni mwa taasisi za kimataifa zinazoshiriki moja kwa moja kwenye kongamano la mwaka huu ni Umoja wa Afrika, ambao umedhamini na kuendesha kikao maalum kilichopewa jina: "Mustakabali wa Uandishi wa Habari barani Afrika."