1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandishi habari washinda tuzo ya amani ya Nobel

Iddi Ssessanga
8 Oktoba 2021

Kamati ya Nobel imewatangaza waandishi habari Maria Ressa wa Ufilipino, na Dmitry Muratov wa Urusi kuwa washindi wa tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka huu wa 2021 kutokana na juhudi zao za kupigania uhuru wa kujieleza.

https://p.dw.com/p/41R7K
Bildkombo-Die Freidensnobel-Preistraeger Maria Ressa und Dmitry Muratov 2021

Akitangaza washindi hao siku ya Ijumaa, Reiss-Andersen amesema "uandishi huru na unaozingatia ukweli unasaidia kulinda dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka, uongo na propaganda za kivita."

"Bila uhuru wa kujieleza na uhuru wa habari", Reiss-Andersen amesema, "itakuwa vugumu kukuza kwa ufanisi, udugu baina ya mataifa, upunguzaji wa nguvu za silaha na kujenga utaratibu bora wa dunia katika zama zetu."

Soma pia: Kamati ya Nobel yatangaza washindi wa tuzo ya amani ya mwaka 2021

Kamati ya Nobel imesema Ressa, mnamo mwaka 2012 alikuwa mwasisi mwenza wa mtandao wa habari wa Rappler, ambao umekuwa msitari wa mbele kukosoa kampeni tata na ya kikatili ya rais wa Ufilipino Rodrigo Durtete, ya kupambana dhidi ya madawa ya kulevya.

Global Media Forum 2020 digital | 
Maria Ressa, chini kushoto, akichangia kwenye mjadala wakati wa jukwa la kimataifa la waandishi habari linaloandaliwa na DW kila mwaka.Picha: DW

Yeye na Rappler, wameandika pia namna mitandao ya kijamii inatumika kusambaza habari za uzushi, kuwanyanyasa wapinzani na kuupotosha umma.

Kwa upande wake, Muratov alikuwa mmoja wa waanzilishi wa gazeti huru la Urusi la Novaya Gazeta mnamo mwaka 1993.

Gazeti hilo ndiyo huru zaidi nchini Urusi hii leo, likiwa na mtazamo wa ukosoaji kwa mamlaka, imesema kamati ya Nobel.

Imeongeza kuwa uandishi wa gazeti hilo unaozingatia ukweli na ueledi vimelifanya kuwa chanzo muhimu cha taarifa kuhusu masuala yanayokosolewa ya jamii ya Urusi ambayo ni nadra kutajwa na vyombo vingine.

Soma pia: Mtanzania Abdulrazak Gurnah ashinda nishani ya Nobel ya Fasihi

Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov, amempongeza Muratov kwa ushindi wa tuzo hiyo, na kumsifu kama mtu mwenye kipaji na jasiri.

Tuzo ya Nobel inalenga kutambua mtu au mashirika ambayo yamafanya kazi bora au kubwa zaidi kwa ajili ya kujenga maridhiano baina ya mataifa.

Tuzo ya mwaka jana ilikwenda kwa shirika la chakula duniani WFP, ambalo lilianzishwa mwaka 1961 kwa agizo la rais wa Marekani Dwight Eisenhower ili kukabiliana na njaa kote duniani.

Dmitri Muratow
Dmitry Muratov, mshindi mwenza wa tuzo ya Amani ya Nobel kwa mwaka huu wa 2021.Picha: Alexander Zemlianichenko/AP Photo/picture alliance

Shirika hilo lenye makao yake mjini Rome Italia, lilisifiwa kwa juhudi zake za kukomesha matumizi ya njaa kama silaha ya kivita na mizozo.

Soma pia: Shirika la Chakula Duniani WFP lashinda Tuzo ya Amani, Nobel

Tuzo hiyo ya kifahari inaambatana na nishani ya dhahabu na pesa taslimu zaidi ya dola za Marekani milioni 1.4.

Zawadi ya pesa hiyo inatoka kwenye urithi ulioachwa na muasisi wa tuzo hiyo, mvumbuzi wa Sweden Alfred Nobel, aliefariki mwaka 1895.

Washindi wengine wa Nobel mwaka huu

Jumatatu wiki hii, kamati ya Nobel ilitoa tuzo ya fiziolojia au utabibu kwa Wamarekani David Julius na Ardem Patapoutian, kutokana na ugunduzi wao juu ya namna mwili wa binadamu unatambua joto na mguso.

Soma pia: Mtanzania Abdulrazak Gurnah ashinda tuzo ya Nobel ya Fasihi

Tuzo ya Nobel katika fizikia ilitolewa Jumanne kwa wanasayansi watatu ambao kazi yao iligundua nidhamu katika hali inayoonekana kukosa nidhamu, na hivyo kusaidia kufafanua na kutabiri nguvu ngumu za kiasili, ikiwemo ufahamu wetu unaopanuka kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Abdulrazak Gurnah | Gewinner Literaturnobelpreis 2021
Mshindi wa tuzo ya Nobel katika fasihi, Mtanzania anaeishi Uingereza Abdulrazak Gurnah.Picha: Frank Augstein/AP Photo/picture alliance

Benjamini List na David W.C MacMillan ndiyo walitunzwa nishani ya kemia Jumatano kwa kugundua njia safi zaidi na rafiki wa mazingira ya kujenga molekyula zinazoweza kutumika kutengeneza mchanganyiko, ikiwemo dawa za kutibu na za kuulia wadudu.

Tuzo ya Nobel katika fasihi ilitolewa jana kwa mwandishi wa Kitanzania mwenye makao yake nchini Uingereza Abdulrazak Gurnah, kwa kutambua kazi zake juu ya athari za ukoloni na hatima ya mkimbizi. Siku ya Jumatatu itatolewa tuzo ya kutambua kazi ya kipekee katika nyanja ya uchumi.

Chanzo: Mashirika