Kipa Enke ameingia katika madaftari ya historia | Magazetini | DW | 16.11.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Kipa Enke ameingia katika madaftari ya historia

Maziko ya Enke kipa wa timu ya Taifa ya Ujerumani na wa klabu ya Hannover 96;matokeo ya mkutano mkuu wa chama cha Social Democratic SPD ni miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani.

Basi tutaanza na gazeti la SCHWÄBISCHE ZEITUNG linalosema:

"Chama cha SPD kimeelewa vizuri adhabu iliyotolewa na wapiga kura wake. Münterfering ameshaondoka,Clement nae hayupo tena chamani na Schroeder wala hakuhudhuria mkutano wa Dresden. Hatimae chama cha SPD ni huru na shukrani ziende kwa mwenyekiti mpya wa chama hicho Sigmar Gabriel anaesimamia pia mfumo wa sera za kisiasa. Na hiyo ni sahihi. Katika mkutano wa Dresden,chama cha SPD kilishughulikia uadilifu wake wa zamani wa kushikamana."

Na gazeti la FRANKFURTER NEUE PRESSE likiendelea na mada hiyo hiyo linasema:

"Mwenyekiti mpya wa SPD Sigmar Gabriel akitazama yale yaliyomkuta mtangulizi wake Schroeder, bila shaka atajiepusha na kosa kuu lililofanywa na mwenzake-kupitisha maamuzi peke yake. Kwa hivyo Gabriel atajaribu kushauriana zaidi na wanachama wenzake. Na hiyo haitokuwa shida kwa vile SPD sasa kipo upande wa upinzani."

Lakini kwa maoni ya gazeti la SÄSCHSISCHE ZEITUNG vigumu zaidi ni kuwa na msimamo mmoja na utakaowavutia wapiga kura. Linaongezea hivi:

"Ni rahisi kutoa wito bila ya kufanikiwa kuwa wamiliki mali watozwe kodi ya matajiri . Lakini si rahisi hivyo kutayarisha sera itakayozingatia jamii ya wazee na itakayowaondoshea hofu ya kuangukia kwenye umasikini huku sera hiyo ikiwa tofauti na ile ya kustaafu baada ya kutimia miaka 67. Chama cha SPD kina mengi ya kutekeleza."

Sasa tunapindukia mada iliyosababisha majonzi makubwa nchini humu. Maziko ya kipa wa timu ya taifa ya Ujerumani Robert Enke. Gazeti la FLENSBURG TAGEBLATT linaeleza hivi:

"Sala badala ya kufurahia goli. Wanaspoti mashuhuri wamelia waziwazi sawa na washabiki wa dimba. Uwanja wa michezo wa Hannover ulijaa maelfu ya watu waliokwenda kumuaga kipa Robert Enke. Ni vema ikiwa kunazingatiwa kufanywa mabadiliko fulani katika kandanda, lakini hayo hayatoshawishi kandanda na biashara kwa muda mrefu, kwani kinachohesabiwa ni magoli na pointi na fedha nyingi sana - fedha ambazo hazikuweza kumsaidia hata Robert Enke."

Kwa kumalizia BADISCHE NEUESTE NACHRICHTEN linasema Enke ameingia katika madaftari ya historia kama shahidi wa mapambano yasio na mwisho.

Mwandishi: P.Martin/DPA

Mhariri: M.Abdul-Rahman