Kikosi cha Marekani Olimpik | Michezo | DW | 23.07.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Kikosi cha Marekani Olimpik

Marekani inapania tena kuipiku Urusi na wenyeji china katika orodha ya medali.

Katika michezo yoyote ya olimpik, kinyan'ganyiro cha dola gani itaibuka na medali nyingi kabisa za dhahabu,fedha na shaba, kimekua kati ya Marekani na Urusi.Mara hii, China, mwenyeji, inataka kuzipiku dola hizo kuu na kuparamia binafsi kileleni hapo August 24 pale bunduki ya mwisho itakapolia kuifunga michezo ya Beijing, inayoanza wiki 2 kutoka sasa hapo August 8.

Ramadhan Ali anakikagua kikosi cha wanariadha wa Marekani katika michezo ya Beijing,ambacho kiliagwa rasmi majuzi na Rais George Bush atakaehudhuria binafsi ufunguzi wa michezo hiyo.►◄

China kama mwenyeji wa michezo ya Beijing,ilianza kujiandaa mara tu ilipokabidhiwa ufunguo wa kuandaa michezo ya 2008.Shabaha yxake haikua tu kuwa mwenyeji na kuwakaribisha kwa mikono 2 wanariadha wake kwa waume kutoka kila pembe ya dunia mjini Beijing, bali pia kama inavyojaribu katika medani ya kisiasa kuibuka pia dola kuu la kispoti ulimwenguni.

Marekani lakini, haitaiachia China kwa urahisi hivyo kuipiku.Pamoja na Urusi, Marekani itatoa changamoto kali ili kurudi nyumbani na medali zaidi kikapuni.

Marekani ilifanya hivyo katika michezo 4 iliopita ya olimpik tena mfululizo wakati wa michezo ya kwanza ya Los Angeles, 1932.

Urusi ikiwa wakati ule Soviet Union iliparamia kileleni mara 8 kuanzia 1956 hadi 1992.Hatahivyo, haikuifikia Marekani.

Wanariadha wa Marekani wameongoza orodha ya medali katika michezo ya Atlanta,georgia, 1996,sydney, Australia, 2000 na miaka 4 iliopita huko Athens, 2004.

Machina mara hii wamepania kuwapiku hata ikibidi kutumia mashabiki wengi wa nyumbani kuwatia shime katika shabaha yao hiyo.

Katika michezo ya Athens, 2004,Marekani iliondoka na jumla ya medali 102 ,na 36 kati ya hizo zikiwa za dhahabu.Warusi walinyakua medali 92 na kati ya hizo 27 zilikuwa za dhahabu huku China ikiridhika mara ile na medali 63, 32 zikiwa za dhahabu.

Marekani iliiibuka na medali 97 katika michezo ya mwaka 200 huko Sydney, Australia kabla malkia wake wa mbio fupi Marion jones kuungama kwamba alidanganya kwa kutumia madawa kutunisha misuli na kuongeza kasi.Matokeo yake alipokonywa medali zake 3 za dhahabu na 2 za shaba.

Katika michezo hii ya Beijing, Mwenyekiti wa Kamati ya olimpik ya Marekani Peter Ueberroth ameapa kupeleka timu safi kabisa mjini Beijing.Tusubiri kuona.

Wakati marekani inatumai kutamba katika medani ya riadha,tumaini kuu la medali linaegemezwa katika hodhi la kuogolea:huko bingwa wake Michael Phelps atazamiwa kutamba tena kwa kunyakua medali nyingi kama vile alivyofanya Mark spitz alietoroka na medali 7 za dhahabu kutoka michezo ya olimpik ya 1972 mjini Munich.Phelps alinyakua medali 6 za dhahabu na 2 za shaba katika michezo iliopita ya olimpik huko Athens,ugiriki.Kwa jumla, Marekani itwaa medali 12 pekee kutoka hodhi la maji.

Kikosi cha Olimpik cha Marekani katika michezo ya Beijing, kinajumuisha pia mabingwa wa gymnastics wa dunia na bingwa wa pande zote Shawn johnson .Pia kuna timu yake maarufu ya mpira wa kikapu Baskeball ambayo mara hii inataka kufuta madhambi iliofanya Athens, miaka 4 iliopita ilipoondokea na medali ya shaba tu.