1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KHARTOUM:Kampuni ya mafuta ya kigeni yatishwa kuondoka

25 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7Cm

Waasi wa Darfur wametangaza kuipa kampuni ya moja ya kigeni ya mafuta wiki moja kujiondoa la sivyo kushambuliwa zaidi baada ya kumteka mfanyikazi mmoja raia wa Canada na mwengine wa Iraq walipovamia kiwanda kimoja cha mafuta nchini humo.

Shambulio hilo lilitokea siku ya jumanne huku mazungumzo ya kutafuta amani ya eneo la Darfur kusubiriwa kuanza tena jumamosi hii nchini Libya.Kundi la waasi la JEM limeshatangaza kuwa linasusia kikao hicho.

Kiwanda hicho cha mafuta kinasimamiwa na kampuni ya mafuta ya Greater Nile Petroleum Operating Company inayohusisha mataifa ya Uchina,India,Malaysia na kampuni ya serikali ya Sudapet.Kwa mujibu wa kamanda wa kundi hilo la waasi yapata viwanda vyengine vinane vilivyokaribu vimefungwa kwa kuhofia kushambuliwa.Uchina kwa upande wake inasema kuwa raia wake wako salama ila wanathibitisha kuwa viwanda hivyo vilishambuliwa.Serikali ya Sudan haijatoa tamko lolote kuhusu tukio hilo.Wakati huohuo Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa linatoa wito kwa makundi yote ya waasi wa Sudan kuhudhuria mkutano wa kutafuta amani unaopangwa kufanyika jumamosi.Mkutano huo unawaleta pamoja waasi na wawakilishi wa serikali ukiwa na lengo la kumaliza ghasia katika eneo la Darfur la Sudan zilizodumu miaka minne u nusu.Baraza hilo linatisha kuchukulia hatua upande wowote utakaohujumu juhudi za kutafuta amani katika eneo hilo.