Kansela Merkel ziarani Japan | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.02.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kansela Merkel ziarani Japan

Kansela Angela Merkel amewasili Tokyo kwa ziara ya siku mbili nchini Japan ambako amepangiwa kukutana na waziri mkuu Shinzo Abe, mfalme Akihito, wanafunzi wa chuo kikuu na viongozi wa makampuni ya kiuchumi ya nchi hiyo.

Kansela Merkel amepangiwa kuzungumza na waziri mkuu Shinzo Abe baadae hii leo, mazungumzo yatakayohusiana na biashara huru, mradi wa nuklea wa Korea ya kaskazini na kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya au Brexit.

Hii ni ziara ya tano ya kansela Merkel nchini Japan na inatokea siku tatu baada ya kuanza kufanya kazi makubaliano muhimu kabisa ya ushirikiano wa kiuchumi, mkataba wa biashara huru kati ya Japan na Umoja wa ulaya. Mkataba huo unajumuisha thuluthi moja ya biashara jumla ya dunia.

 Duru za serikali ya Ujerumani zinasema kansela Merkel na mwenyeji wake waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe wanatarajiwa pia kuzungumzia baadhi ya masuala ya masilahi ya pamoja mfano wa digitali, nishati mbadala na mabadiliko ya mfumo wa maisha katika jamii.

Kesho kansela Merkel amepangiwa kukutana na mfalme mkongwe wa miaka 85, aliyeamua kulivua taji lake April 30 inayokuja, tukio la aina pekee kuwahi kushuhudiwa tangu miaka 200 iliyopita nchini humo. Kansela Merkel atakutana pia na mrithi wa kiti cha ufalme, Mwanamfalme Naruhito atakayekabidhiwa wadhifa huo May mosi inayokuja.

Wajapan na simu zao za mkononi

Wajapan na simu zao za mkononi

 Simu ya mkononi yenye uwezo wa kushika nafasi ya akili ya binaadam

Katika ziara hii ya siku mbili kansela Merkel  atakutana pia na wanafunzi katika chuo kikuu cha Keio mjini Tokyo.

Ratiba ya mwisho katika ziara hii ya kansela Merkel nchini Japan itakuwa kulitembelea kampuni linaalotengeneza mfumo mpya wa simu za mkononi za kiwango cha 5G zinazosemekana kushika nafasi ya akili ya mwanaadam.

Kansela Angela Merkel anafuatana na ujumbe wa wanavianda kutoka sekta tofauti, ikiwa ni pamoja na vile vya elektroniki, madawa na shughuli za fedha.

Japan ni mshirika muhimu wa kibiashara wa Ujerumani. Biashara kati ya nchin hizo mbili imefikia jumla ya Euro bilioni 42.5 mwaka 2017 kutoka Euro bilioni 37.2 mwaka 2015. Makampubni 400 ya Ujerumani yanaendesha shughuli zao nchini Japan.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com