Kansela Merkel atunukiwa medali na Rais Obama | Habari za Ulimwengu | DW | 08.06.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

Kansela Merkel atunukiwa medali na Rais Obama

Rais Barack Obama wa Marekani amemtunukia Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel medali ya uhuru inayotolewa na rais wa Marekani, ambayo ni ya juu kabisa ya kiraia.

default

Rais Barack Obama akimtunuku medali Kansela Angela Merkel

Rais Obama alimtunuku Kansela Merkel medali hiyo wakati wa chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa heshima ya Merkel kama mtu wa kwanza wa Ujerumani Mashariki kuongoza juhudi za kuungana tena Ujerumani baada ya kuanguka kwa utawala wa kikomunisti katika Ulaya Mashariki na kujihusisha kwake na masuala ya uhuru. Akimkabidhi medali hiyo, Rais Obama alisema Bibi Merkel alijiunga na siasa ambapo hadhi yake ilipanda na hatimaye kuweka historia ya kuwa kansela wa kwanza mwanamke nchini Ujerumani na kupaza sauti yake kwa ufasaha katika kutetea haki za binaadamu na utu ulimwenguni kote.

USA Barack Obama Angela Merkel vor dem Weißen Haus in Washington Flash-Galerie

Kansela Merkel akizungumza kwenye bustani ya Whitehouse

Glasi na mawaridi

Rais Obama na Kansela Merkel waligonganisha glasi zao katika chakula hicho cha jioni kilichoandaliwa kwenye ikulu ya Marekani, kilionyesha ishara ya uhusiano wa kirafiki kati ya Marekani na Ujerumani. Akimshukuru Rais Obama kwa medali hiyo, Kansela Merkel alikumbuka enzi za utoto wake katika Ujerumani Mashariki, akisema hakuwahi kufikiria kama siku moja atasimama katika bustani ya mawaridi ya ikulu ya Marekani na kutunukiwa medali hiyo ya heshima na rais wa Marekani.

Barack Obama im Weißen Haus Unterschrift Automat Flash-Galerie

Rais Barack Obama akiwa kwenye Ikulu ya Whitehouse

Msimamo wa pamoja

Bibi Merkel alisema kuwa anaiona medali hiyo ya uhuru inayotolewa na rais wa Marekani, kama ushahidi wa ushirikiano mzuri kati ya mataifa hayo mawili. Aliongeza kusema kuwa nchi zao zinasimama pamoja kwa ajili ya amani na uhuru. Mapema jana Rais Obama alikutana na Kansela Merkel ambapo walijadiliana kuhusu masuala mengi ya kimataifa. Kansela Merkel na Rais Obama waliweka kando tofauti zao hasa kuhusu Libya. Akitolea mfano hatua ya hivi karibuni ya Ujerumani kukataa kushiriki kijeshi katika mpango unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, Rais Obama alisema: ''Kwa kuizingatia Libya nimegundua kuwa hatua ya Ujerumani kupeleka rasilimali zaidi na wanajeshi nchini Afghanistan kumeruhusu washirika wengine wa NATO kuongeza msaada wao katika kikosi kinachowalinda watu wa Libya. Kansela na mimi tumekuwa wazi:Gaddafi lazima ajiuzulu na kukabidhi madaraka kwa watu wa Libya na shinikizo litaongezeka hadi atakapofanya hivyo.''

Merkel / Obama / Freiheitsmedaille / USA / Washington

Kwenye mkutano na waandishi wa habari

Mualiko mwengine

Kwa upande wake Kansela Merkel alisema Ujerumani itakuwa na jukumu kubwa katika kuifufua Libya, pindi kiongozi wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi atakapoachia madaraka. Kuhusu deni la Ugiriki, Rais Obama aliyataka mataifa ya Ulaya, hasa Ujerumani kuzuia kosa lolote kutoka kwa Ugiriki. Bibi Merkel pia alipata chakula cha mchana katika wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani kilichoandaliwa na Makamu wa Rais, Joe Biden na waziri wa wizara hiyo, Hillary Rodham Clinton.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE)

Mhariri:Josephat Charo

DW inapendekeza

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com