1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KAMPALA : Nchi zalalamikia repoti juu ya Somalia

18 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCrc
Rais Parvez Musharaf wa Pakistan
Rais Parvez Musharaf wa PakistanPicha: AP

Uganda imesema hapo jana italalamika kwa Umoja wa mataifa juu ya repoti yenye kuishutumu nchi hiyo pamoja na nchi nyengine tisa kwa kuwapa silaha na kutuma vikosi kuunga mkono makundi hasimu katika mzozo unaotokota nchini Somalia.

Waziri wa Ulinzi wa Uganda Chrispus Kiyonga amewaambia waandishi wa habari kwamba repoti hiyo ni upuuzi mtupu na Uganda sasa italalamika rasmi kwa Umoja wa Mataifa juu ya repoti hiyo nzito,mbaya na ya uzushi.

Kiyonga alitowa kauli hiyo kufuatia repoti ya uchunguzi wa Umoja wa Mataifa yenye kuitaja Uganda sambamba na Ethiopia kuwa ni nchi zenye kupelekea silaha,wanajeshi na zana kwa serikali dhaifu ya mpito nchini Somalia katika mzozo wake na Uongozi wa Kiislam wenye kuudhibiti mji mkuu wa Mogadishu.

Nchi nyengine zikiwemo Libya,Misri na Yemen zinashutumiwa kwa kuunga mkono Uongozi wa Mahkama za Kiislam.

Libya imetupilia mbali repoti hiyo kwa kusema kwamba haina msingi na kuwa kinyume chake nchi hiyo imekuwa ikitimiza dhima muhimu ya kutafuta amani nchini Somalia kwa miaka mingi. Misri ambayo imeshutumiwa kwa kuwapa mafunzo wanamgambo wa Kiislam imesema repoti hiyo haina ukweli hata kidogo na kuwa inaonyesha kutoielewa kabisa sera ya Misri kwa Somalia.

Repoti hiyo ya Umoja wa Mataifa kuhusu ukiukaji wa vikwazo vya silaha uliowekwa kwa Somalia hapo mwaka 1992 imezitaja nchi 10 na makundi ya wanamgambo kwa kuyapatia silaha,zana na mafunzo makundi yanayohasimiana katika mzozo wa Somalia.