1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSyria

Jeshi la Syria lazidiwa, laikimbia Aleppo

30 Novemba 2024

Jeshi la Syria lilisema Jumamosi kuwa dazeni kadhaa ya wanajeshi wake waliuwawa kufuatia shambulizi lililofanywa kaskazini magharibi mwa Syria.

https://p.dw.com/p/4nbU3
Wanamgambo wa upinzani Syria wakiwa Aleppo
Wanamgambo wa upinzani Syria wakiwa AleppoPicha: ABDULAZIZ KETAZ/AFP

Jeshi hilo lilisema pia kwamba waasi walifanikiwa kuingia sehemu kubwa ya mji wa Aleppo hatua iliyolilazimu jeshi kuondoka mjini humo.

Taarifa hiyo ya jeshi la Syria ndiyo tamko la kwanzala jeshi kukiri kwamba wanamgambo wanaoongozwa na waasi wa Kiislamu wa Hayaz Tahrir al-Sham, wameingia katika mji huo wa Aleppo uliokuwa chini ya serikali, katika shambulizi la kushtukiza lililoanza mapema wiki hii.

Jeshi la Syria lashambulia maeneo ya waasi kwa mabomu

"Idadi kubwa ya magaidi na maeneo mengi ya mapigano yamesababisha vikosi vyetu vya jeshi kuondoka kwa lengo la kuimarisha maeneo ya ulinzi, ili kukabiliana na shambulizi hilo, kuyalinda maisha ya raia na kujiandaa kwa shambulizi la kulipiza kisasi," ilisema taarifa ya jeshi.

Magari yakichomwa moto na wanamgambo Aleppo
Magari yakichomwa moto na wanamgambo AleppoPicha: OMAR HAJ KADOUR/AFP

Shambulizi hilo la waasi ndiyo changamoto kubwa katika kipindi cha miaka kadhaa kwa Rais Bashar al-Assad na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo ambavyo kwa sehemu kubwa vimepoa tangu mwaka 2020.

Taarifa hiyo ya jeshi la Syria ilisema kuwa waasi hao hawajaweza kuwa na sehemu maalum mjini Aleppo kutokana na hatua ya jeshi la Syria kuyashambulia mara kwa mara maeneo yao kwa mabomu.

Vyanzo viwili vya jeshi la Syria mapema vilisema kwamba ndege za kivita za Urusi na Syria ziliwalenga waasi katika mtaa mmoja wa Aleppo Jumamosi.

Urusi ililipeleka jeshi lake la anga nchini Syria mwaka 2015 kumsaidia Assad kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria, vilivyoanza mwaka 2011.

Ukiukwaji wa uhuru wa Syria

Waasi nao walianza mashambulizi yao mapema wiki hii, wakishambulia miji iliyo chini ya udhibiti wa serikali na kufika Aleppo, karibu mwongo mmoja baada ya jeshi la Syria likiungwa mkono na vikosi vya Urusi na Iran, kuwatimua waasi kutoka mji huo.

Wapiganaji wa upinzani wakiandaa kombora
Wapiganaji wa upinzani wakiandaa komboraPicha: Anas Alkharboutli/dpa/picture alliance

Akizungumza Ijumaa, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema Urusi inayachukulia mashambulizi hayo ya waasi kama ukiukwaji wa uhuru wa Syria.

"Tungependelea mamlaka nchini Syria zirudishe utulivu na kuheshimiwa kwa katiba haraka iwezekanavyo," alisema Peskov.