Je, Iran ilikuwa na mazungumzo na Israel | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.10.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Je, Iran ilikuwa na mazungumzo na Israel

Mashariki ya Kati bila nuklia ?

Mahmoud Ahmadinejad

Mahmoud Ahmadinejad

Wizara ya nje ya Israel pamoja na Shirika la Nguvu za Atomiki la Israel,imethibitisha adhuhuri ya leo, ripoti ya gazeti la kila siku la Israel "Ha'aretz" kuwa bingwa wa atomiki wa kiisraeli wakati wa mkutano wa siku 2 mjini Kairo, mwishoni mwa mwezi uliopita wa Septemba ,alizungumza na maafisa rasmi wa Iran juu ya uwezekano wa kuwa na eneo huru la Mashariki ya Kati lisilo na silaha za kinuklia.

Kwa muujibu wa gazeti hilo la Ha-aretz,haukua mkutano wa pande hizo mbili, bali kilikua kikao cha kwanza kati ya wajumbe wa serikali hizo mbili tangu mapinduzi ya kiislamu ya Iran,1979.Iran kwa upande wake, inakanusha kufanya mazungumzo ya aina hiyo na Israel na inasema huo ni uzushi mtupu.

Msemaji wa Tume ya nishati ya nguvu za Atomiki ya Israel (IAEC) Yael Doron,ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kuwa, mjumbe wa Tume hiyo ya Israel alikuwa na mikutano kadhaa na afisa wa kiirani kuzungumzia maswali ya kimkoa chini ya usimamizi wa Australia.Iran lakini, inakanusha hayo.

Doron alikataa kutoa maelezo zaidi juu ya mikutano hiyo lakini, gazeti la Ha-aretz limeripoti kuwa, maafisa wa pande hizo mbili walizungumzia nafasi za kuitangaza Mashariki ya Kati kuwa eneo lisilo na silaha za nuklia.Hii ilikua wakati wa kikao chao cha hapo Septemba mwaka huu, cha kwanza kabisa tangu Shah wa Iran kupinduliwa 1979.

Haraetz likasema kuwa, mkurugenzi wa Tume ya Nguvu za Atomiki ya Israel (IAEC) anaehusika na sera na upunguzaji silaha, Meirav Zafary-Odiz na mjumbe wa sasa wa Iran katika Shirika la nguvu za Atomiki Ulimwenguni (IAEA) Ali Asghar Soltanieh,walikutana mara kadhaa mjini Cairo, mwishoni mwa mwezi uliopita.

Katika mkutano walikuwa wajumbe wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu-Arab League,Jordan,Misri,Tunisia,Morocco,Umoja wa Falme za Kiarabu (Emirates) na Saudi Arabia na hata maafisa wa Umoja wa Ulaya na Marekani.

Gazeti likaongeza kusema kuwa, mkutano huo ulifanyika chini ya usimamizi wa Tume ya ulimwengu juu ya kuzuwia kuenezwa kwa silaha za kinuklia-tume ambayo iliasisiwa kwa juhudi ya waziri-mkuu wa Australia,Kevin Rudd.

Iran ikikanusha hayo inadai hivi ni vita vya kiakili venye shabaha mafanikio inayopata Iran mara kwa mara katika diplomasia yake tangu kwenye mikutano ya Geneva hata ile ya mjini Vienna.

Israel, dola pekee la kinuklia lisilojitapa hadharani kumiliki silaha hizo huko Mashariki ya kati haikuwahi kuficha kutumia nguvu za kijeshi kuzuwia mradi wa kinuklia wa Iran ambao kambi ya magharibi inaitilia shaka Iran kuwa nao. Teheran inakanusha.

Taarifa zasema kuwa, katika mkutano mmoja huko Cairo,Misri, mjumbe wa Iran Soltanieh alimuuliza mjumbe wa Israel, Zafary-Odiz: "Mnazo au hamna silaha za nuklia ?"-Gazeti la Ha-aretz limeripoti likiegemeza taarifa zake kutoka mjumbe asietajwa aliekuwapo mkutanoni. Muisraeli huyo alicheka tu,hakujibu.

Soltanieh, alisema kuwa, Iran haitaki kuunda silaha za kinuklia na hivyo, haiihatarishi Israel. Akaongeza kusema kwamba, Iran haiwachukii wayahudi bali inaupinga uzayouni.

Mwandishi: Verenkotte, Clemens/ZR/Ali Ramadhan

Mhariri:M.Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com