1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yapinga kuwa na maelewano na Chama cha Hamas kuhusu Ukanda wa Gaza.

Scholastica Mazula12 Machi 2008

Waziri wa Ulinzi wa Israel Ehud Barak, amesisitiza kwamba hakukuwa na makubaliano baina ya Israel na kundi la Hamas .

https://p.dw.com/p/DNUW
Moshi ukionekana kutoka Mashariki mwa Ukanda wa Gaza baada ya Israel kufanya mashambulizi ya anga kutokea Kusini Mashariki mwa Israel, March 1, 2008. ambapo watu arobaini na saba waliuawa wengi wao wakiwa ni raia wa kawaida.Picha: AP

Aidha ameonya kuwa Israel itaendelea na mashambulizi endapo makombora ya maroketi yataendelea kuvurumishwa katika Ukanda wa Gaza.

Waziri huyo wa ulinzi wa Israel ameiambia Radio ya Taifa ya Israel kwamba wataendelea na mapigano kwa lengo la kupinga mashambulizi hayo ya maroketi ambayo yamekuwa yakivurumishwa kutoka Ukanda wa Gaza na watahakikisha yanamalizika japo halitakuwa suala la kumalizika kwa siku moja.

Akiwa katika kituo cha majeshi ya Israel karibu na mpaka wa Ukanda wa Gaza, Barak amesisitiza kwamba wanatarajia kufanya operesheni nyingine hivi karibuni na kampeni yao dhidi ya Gaza inaweza kusababisha hatari pia katika maeneo mengine.

Hata Hivyo kiongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniya, amesema kwamba Israel inatakiwa kuchukua hatua nyingine endapo inataka maelewano ya kweli katika ukanda wa Gaza na maeneo mengine ambayo yanazungukwa na kundi la Waislamu wenye itikadi kali wa chama cha Hamas.

Haniya ambaye ni waziri Mkuu katika Serikali ya chama cha Hamas alifukuzwa madarakani na Serikali ya Rais wa Palestina Mahmud Abbas baada ya chaama cha Hamas kuuchukua Ukanda wa Gaza kwa nguvu mwezi Juni mwaka 2007.

Akihutubia katika chuo kikuu cha kiislam ,Ismael Haniya amesema "maakubalian yoyote ya kusitisha mapigano lazma yawe kwa ridhaa za pande zote na kuheshimiwa wakati mmoja na pande zote.

Ismael Haniya amesisitiza kwa mara nyengine tena ikiwa Israel itaridhia kukomesha uvamizi na kuondowa vizuwizi vilivyowekwa Gaza tangu Hamas walipotwaa madaraka,wanamgambo wa kipalastina watakutana ili kushauriana na kutoa jibu sahihi kwa ajili ya mpango wa kuweka chini silaha.

Misri imekua ikisimamia mazungumzo katika juhudi za kufikiwa makubaliano ya kumaliza matumizi ya nguvu ndani na nje ya Gaza pamoja na kulitoa eneo hilo kutoka hali ya upweke eneo hilo la wapalastina.

Maafisa wa Israel wamekanusha hadharani aina yoyote ya kuweko mashauriano kuhusu masuala hayo-ingawa wamekubali juhudi zinaendeshwa.

Maafisa wa misri nao pia wamethibitisha juhudi zinaendelezwa kusaka ufumbuzi wa kina.

Juhudi hizi mpya zinafuatia matumizi ya nguvu ya siku tano mfululizo,baada ya wapalestina 130 na Waisrael 5 kuuliwa mwishoni mwa mwezi uliopita.

Wakati huo huo serikali ya Israel imesema inaisusia televisheni ya Al Jazeerra,ikilalamika dhidi ya kile inachokiita "ripoti zinazoelemea upande mmoja kuhusu Gaza."

Naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Israel Majali Wahbe, amesema Aljazeerra inatoa habari nusu nusu na inawaunga mkono magaidi .Israel imetuma Taarifa ya malalamiko kwa wakuu wa kituo hicho cha televisheni ya kiarabu.