1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel: Hakutakuwa na utulivu Lebanon bila usalama Israel

26 Novemba 2025

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz ameonya kuwa hakutakuwa na utulivu Lebanon kama Israel haitahakikishiwa usalama wake.

https://p.dw.com/p/54JY9
Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz
Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel KatzPicha: Handout/dpa/picture alliance

Katz ameongeza pia kuwa Israel haitoruhusu vitisho dhidi ya wakaazi wake katika eneo la kaskazini.

Ameitoa kauli hiyo leo bungeni wakati vikosi vya Israel vikiendeleza opereshenizake kusini mwa Lebanon, licha ya makubaliano ya kusitisha vita na kundi la Hezbollah yaliyofanyika mwaka moja uliopita.

Wakati huo huo, jeshi la Israel limearifu kuwa limewaua Wapalestina sita kwa kile ilichokitaja kuwa "kufanya ugaidi" katika mji wa Rafah.

Limesema pia kuwa watu hao waliuawa wakati wakitokea kwenye handaki walilolitumia kama maficho yao.

Na katika hatua nyingine Israel imeirejesha miili ya Wapalestina 15 Ukanda wa Gaza muda mfupi baada ya mabaki ya mwili wa mateka wa Israel kurudishwa nyumbani.

Wizara ya Afya ya Gaza iliyo chini ya Hamas imethibitisha kuwasili kwa miili hiyo ambayo tayari imeshatambuliwa.

Kurejeshwa kwa miili hiyo ni sehemu ya makubaliano ya kusitisha vita kati ya Israel na Hamas yanayojumuisha kubadilishana mateka walio hai na wafu.