IS yaiteka kambi ya jeshi la anga Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

IS yaiteka kambi ya jeshi la anga Syria

Kundi linalojiita Dola la Kiislamu-IS limeikamata kambi muhimu ya jeshi la Syria ambayo ilikuwa ngome ya mwisho ya jeshi hilo katika jimbo la al-Raqqa. Naye mwandishi wa habari wa Marekani aliyetekwa Syria ameachiwa

Hayo yanaarifiwa wakati mwandishi habari wa Marekani aliyekamatwa na kushikiliwa mateka kwa karibu miaka miwili na wanamgambo nchini Syria akiwa ameachiwa huru, wiki moja tu baada ya wanamgambo wenye itikadi kali za kiislamu kutoa video iliyoonyeshwa wakimchinja mwandishi mwa habari Mmarekani James Foley.

Akithibitisha habari za kuachiwa kwa mwandishi huyo, mshauri wa usalama wa taifa katika Ikulu ya Rais nchini Marekani Bibi Susan Rice amesema mmarekani huyo aliyeachiliwa huru ni Peter Theo Curtis mwenye umri wa miaka 45 kutoka jimbo la Massachusetts. Bibi Rice amesema Curtis kwa sasa ameondolewa nchini Syria na yuko salama.

Video Still Al Jazeera Theo Curtis Journalist Syrien

Peter Theo Curtis aliyeshikiliwa mateka na wanamgambo nchini Syria kwa Karibu miaka miwili

Waziri wa Mambo ya nchi za Kigeni wa Marekani John Kerry amesema Curtis alishikiliwa na kundi la Jabhat al-Nusra, linalofahamika pia kama al-Nusra Front, ambalo ni tawi la mtandao wa al-Qaeda nchini Libya linalopigana na serikali ya Bashar al-Assad.

Inaaminika kuwa Curtis hakuwa miongoni mwa mateka wanaoshikiliwa na kundi la Dola la Kiislamu – IS ambalo lilimuua Foley. Rais Barack Obama alijulishwa kuhusu habari hizo wakati akimalizia likizo yake katika jimbo la Massachusetts.

Rais Obama amesema Marekani itaendelea kutumia uwezo wake wote katika kuhakikisha kuwa raia wake waliosalia mikononi mwa watekaji wanaachiliwa huru. Curtis aliachiliwa katika eneo la Milima ya Golan, ambako alikabidhiwa maafisa wa serikali ya Marekani waliomsafirisha hadi Tel Aviv. Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Qatar ilithibitisha kuwa serikali ya nchi hiyo ndiyo iliyoongoza juhudi za kuachiliwa mwandishi huyo wa habari.

Habari za kuachiliwa kwake zimekuja siku chache tu baada ya video kujitokeza katika mtandao wa intaneti, ikimwonyesha mwanahabari mwingine wa Marekani James Foley akichinjwa, na mpiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu – IS

Flughafen von Tabka von ISIS eingenommen

Wanamgambo wa Dola ya Kiislamu wameuteka mji wa Tabqa pamoja na kambi ya jeshi la Syria

Balozi wa Uingereza nchini Marekani Peter Westmacott amesema maafisa wa Uingereza wanakaribia kumtambua mtu aliyejifunika uso wake ambaye alionekana kwenye video hiyo akimchinja James Foley.

Wakati huo huo, wapiganaji wa IS wameivamia kambi ya jeshi la anga la Syria ya Tabqa na kuchukua udhibiti wa kambi hiyo iliyokuwa ngome ya mwisho ya serikali katika mkoa wa kaskazini mashariki wa al-Raqqa. Shirika la kutetea haki za binaadamu la Syria lenye makao nchini Uingereza limesema majeshi ya serikali yaliondoka katika uwanja huo na kukimbilia jangwani. Shirika la habari la serikali ya Syria- SANA, limesema jeshi la Syria lilifanya operesheni iliyofanikiwa ya kujiimarisha upya baada ya kuondoka katika uwanja huo wa ndege na linaendelea kuwashambulia magaidi katika eneo hilo.

Shirika la haki za binadamu la Syria limesema zaidi ya watu 500 wameuawa katika makabiliano ya kuitwaa kambi hiyo ya Tabqa. Takribani wanamgambo 346 wenye msimamo mkali wameuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa tangu Dola la Kiislamu lilipoanzisha mashambulizi dhidi ya kambi hiyo Jumanne wiki iliyopita. Shirika la haki za binadaamu la Syria limesema zaidi ya wanajeshi 170 wa Syria waliuawa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Gakuba Daniel

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com