Iraq: Usalama baada ya Wamarekani kuondoka mijini | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.07.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Iraq: Usalama baada ya Wamarekani kuondoka mijini

Jee, majeshi ya Iraq yataweza kurejesha amani nchini?

Bendera za Marekani na Iraq juu ya ramani ya Iraq

Bendera za Marekani na Iraq juu ya ramani ya Iraq

Tarehe 30 mwezi Juni uliopita, ilianza enzi mpya nchini Iraq. Hiyo ilikuwa ni siku ya mwisho kwa wanajeshi 131,000 wa Kimarekani katika nchi hiyo kuondoka kutoka miji mikubwa. Wachunguzi wanasema siku hiyo inaweza ikachukuliwa kuwa ni mwanzo wa hatima ya uvamizi wa Marekani uliodumu miaka sita sasa katika nchi hiyo ya Kiarabu. Na hadi Agosti 31 mwaka 2010, inatarajiwa kwamba sehemu kubwa ya wanajeshi wa Kimarekani walioko Iraq watakuwa wamesharejea nyumbani. Mwanajeshi wa mwisho wa Kimarekani ataondoka mwisho wa mwaka 2011. Hali hiyo inazusha suali kama Iraq, kweli, kutokana na nguvu zake yenyewe, inaweza kuwa na usalama na utulivu?

Hatua hiyo iliochukuwa Marekani kuondosha wanajeshi wake kutoka miji mikubwa ya Iraq ni ishara muhimu katika ile njia ndefu, na huenda ikafurika kwa damu, kuelekea Iraq kuwa na mamlaka kamili ya utawala wake tangu pale Wamarekani walipofanya uvamizi mwaka 2003. Uvamizi huo ulipelekea kupinduliwa kutoka madarakani mdikteta Saadam Hussein, lakini pia ukasababisha kuweko ugaidi na vitendo vya matumizi ya nguvu baina ya makabila na madhehebu ya nchi hiyo inakopitia Mito ya Euphrates na Tigris.

Siku hiyo ya Juni 30 iliadhimishwa na kusheherekewa kwa mbwembwe, kukiweko paredi za kijeshi, tamasha za muziki na kupigwa magoma mabarabarani katika mji mkuu wa Baghdad na miji mengine. Waziri mkuu Nouri al-Maliki hapo kabla aliizungumzia hatua hiyo kuwa ni ushindi mkubwa, licha ya kwamba wakati anazungumza hayo mashambuluio kadhaa yalifanyika siku chache kabla na kuchukuwa roho za zaidi ya watu 200.

Hivi sasa wanajeshi wa Ki-Iraqi wanatakiwa waonekane kila mahala, na tangu jumanne iliopita mji mkuu wa Baghdad umekuwa ukilindwa na wanajeshi 130,000, licha ya kuweko pia polisi 180,000. Kwa ujumla, Iraq itakuwa na polisi nusu milioni na wanajeshi robo milioni ili kuhakikisha usalama unakuweko. Wanajeshi na magari ya kivita ndio itakuwa picha inayoonekana katika mabarabara ya miji ya Iraq, na kwa kawaida majeshi ya Kimarekani hayataonekana katika miji hiyo.

Hasa wanasiasa wengi wa kutoka madhehebu ya Shia yalio na watu wengi katika nchi hiyo wamefurahishwa na tangazo la kuondoka wanajeshi wa Kimarekani kutoka miji mkubwa, licha ya kwamba Waarabu wa madhehebu ya Shia ndio waliofaidika sana kutokana na kuondoshwa madarakani Saadam Hussein. Kinyume na hayo, watu wengi wa madhehebu ya Sunni wana wasiwasi, licha ya kwamba Wamarekani wameweza kuleta utulivu katika mikoa iliokuwa na michafuko na inayokaliwa na Wasunni wengi. Wamefanya hivyo kwa kuyaunganisha makabila ya mikoa hiyo. Idadi ya mashambulio na idadi watu waliokufa imepunguwa, ukilinganisha na kilele kilichofikiwa hapo mwaka 2006.


Wabunge wengi wa Iraq wana matumaini, kama vile anavosema mbunge wa madhehebu ya Shia, Ayad Jamaleldin, licha ya mashambulio kadhaa yaliofanywa wiki iliopita. Wao wana hakika kwamba majeshi ya Iraq yana uwezo na yako tayari kuwalinda raia wa nchi hiyo.

" Bila ya shaka, majeshi ya Iraq yana uwezo wa kuhakikisha usalama katika miji. Yana uwezo zaidi kuliko majeshi ya kimataifa, kwa vile yanaweza kwa uzuri na kwa haraka zaidi kuwatambuwa watu. Pia wanaijuwa vizuri zaidi jiografia ya nchi hii."

Vivyo hivyo, ndivyo anavoona mbunge wa madhehebu ya Kisunni, Shadha al Abussi:

" Tuna imani kubwa na wanajeshi wetu. Naamini kwamba ikiwa kila raia atachangia katika kuidhibiti hali ya mambo katika Iraq, basi tunaweza kupata mafanikio makubwa zaidi."

Kwamba mitihani ilioko mbele ni mikubwa na migumu, ni jambo linalotambuliwa na wabunge hao wawili. Kutokana na fikra za mbunge Ayad Jamaleldin ni kwamba mitihani hiyo haitokani tu na mikwaruzano na mapambano ya kuwania madaraka baina ya makundi tafauti ya kisiasa, kikabila na kidini, lakini pia ushawishi unaojipenyeza kutoka nchi jirani.

Mbunge Ayad Jamalildin...

"Mtihani mkubwa uko ndani ya nchi, katika uwanja wa kisiasa, na katika kujiingiza madola ya kimkoa katika mambo ya ndani ya Iraq."

Iran, Syria, Saudi Arabia na nchi nyingine zinajitahidi kuzidisha ushawishi wao katika Iraq, na mara nyingi zinashindana katika jambo hilo. Na ni siri ilio wazi kwamba nchi hizo hugawa fedha zitririke kwa makundi yalio na siasa kali ili kuleta michafuko katika nchi hiyo, kupitia vitendo vya matumizi ya nguvu, au angalau kuutia katika majaribio uwezo wa majeshi ya usalama ya nchi hiyo.

Wabunge wengi, kwa hivyo, wanataka mizozo ya kuwania madaraka isuluhishwe kwa kuweko mdahalo wa kikweli na kuweko mpango wa kuliendeleza taifa la Iraq, usiotia maanani maslahi ya vyama vya kisiasa. Ni matarajio ya wabunge hao kwamba kwa kufanya hivyo ushawishi wa madola ya nje ya kimkoa katika nchi hiyo utapunguwa.

Kujongeleana kwa makundi tafauti ambayo yamebakia kutoaminiana kutokana na vitendo vya matumizi ya nguvu vilivojiri miaka sasa kutasababisha uchumi kupata nguvu na hivyo neema kuwamiminikia watu wengi. Hilo ni jambo muhimu, anasema mbunge Ayad Jamaleldin:

"Ni sawa. Uchumi wetu kwa sasa unategemea kabisa mapato ya mafuta, hatuna njia nyingine ya kujipatia fedha. Lakini matarajio ya baadae, kwa fikra yangu, ni mazuri, kwa sharti, lakini, kwamba kutayarishwe mpango wa maendeleo ambao, kwa kweli, utakuwa wa umoja wa taifa na utakaokubaliwa na vyama vyote."

Iraq hivi sasa inatoa mapipa milioni 2.4 ya mafuta kila siku, lakini kima hicho hakifikii kile kilichokuwa kikichimbwa kabla ya Wamarekani kuivamia nchi hiyo hapo mwaka 2003. Wakati huo huo, Iraq ni nchi ya tatu yenye akiba kubwa kabisa ya mafuta duniani. Lakini uchimbuaji wa mafuta ya kutosha unashindikana kutokana na sababu mbali mbali, ikiwa ni pamoja na madeni ya zamani ambayo Iraq inadaiwa na nchi za nje, wasiwasi kutoka upande wa makampuni ya kigeni ya kuchimbua mafuta, biashara ya mágendo ya mafuta na pia kuibiwa mafuta kutoka kwenye mabomba kunaokofanywa na wababe wa kienyeji na wanamgambo.Pia hasa kunakosekana makubaliano ya mwisho baina ya mikoa na makabila yote juu ya mgawo ulio wa haki wa fedha zinazotokana na uuzaji wa mafuta. Na mabishano baina ya Wakurd na Waarabu juu ya nani audhibiti mji wa Kirkuk ulioko kaskazini mwa Iraq bado hayajatanzuliwa.

Watu wengi wanasema kwamba Marekani itabidi iendelee na kujishughulisha na nini kinafanyika Iraq. Zaidi ni kwamba majeshi ya Kimarekani sio kwamba kwa sasa yataondoka kabisa kutoka nchi hiyo, lakini yatawekwa karibu na miji mikubwa, ambako yatakuwa katika hali ya tayari tayari, na angalau sehemu yao kubakia nchini hadi mwisho wa mwaka 2011. Mbunge al-Abussi, kwa hivyo, ana matumaini haya:

"Kurejea nyuma kwa majeshi ya Marekani lazima kutafsiriwe vilivyo. Hiyo ina maana ya kuondoka wanajeshi wa Kimarekani kutoka miji ya Iraq, na hiyo haina maana: kuondoka Marekani kutoka mwenendo wa kisiasa wa Iraq."

Licha ya ya kuwa na imani na majeshi ya Iraq pamoja na mwenendo wa kuliunganisha taifa, mbunge Shadha Al-Abussi anasema wazi kwamba mustakbali wa mambo hayo anauona ni wenye kumpa faraja.

 • Tarehe 08.07.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ijs5
 • Tarehe 08.07.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ijs5
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com