Polisi TZ yadaiwa kutumia nguvu wakati wa uchaguzi
19 Machi 2026
Ripoti ya Human Rights Watch (HRW), imeeleza hali ya kusikitisha iliyoikumba taifa hilo la Afrika Mashariki na kusababisha maafa ya mamia ya watu wakati na hata baada ya uchaguzi nchini humo.
Takwimu za HRW zinaonesha kuwa, watu 31 ambao hawakuwa sehemu ya maandamano waliuawa, huku vifo vya wengine 19 pia vikinakiliwa kufuatia machafuko yaliyoikumba Tanzania.
Shirika hilo limesema kwamba, mamia ya watu waliuawa huku likiitaka tume iliyoundwa na serikali kuchunguza vurugu za uchaguzi ifanye uchuguzi wa kina kuhusu matukio hayo ya ukiukaji wa haki za binadamu na kuwawajibisha wahusika.
Mtafiti katika shirika hilo Oryem Nyeko, amesema kuwa hatua zilizochukuliwa na mamlaka za Tanzania kukandamiza upinzani wakati wa uchaguzi, zilisababisha madhara makubwa kwa maisha ya raia wengi. Ameitaka tume ya uchunguzi kuhakikisha haki inapatikana kwa waathiriwa, kuwawajibisha waliohusika, na kuhakikisha kuwa ukiukaji kama huo hautajirudia tena.
Vizuizi barabarani vyawakwamisha waliojeruhiwa kufika hospitali
Mashahidi waliiambia Human Rights Watch kwamba, wanajeshi na polisi waliweka vizuizi vya barabarani na kuwazuia waliojeruhiwa kufika hospitalini. Baadhi ya watu walifariki kutokana na kukosa huduma ya dharura.
Kati ya Oktoba 2025 na Februari 2026, Human Rights Watch ilihoji jumla ya watu 48 katika mikoa ya Arusha,Dar Es Salaam, Geita,Mwanza, Ruvuma na Zanzibar. Waliohojiwa ni pamoja na mashahidi 34, wanahabari 7, wanaharakati na wanachama wa mashirika 5 ya kiraia.
Mamlaka za Tanzania ziliwakamata zaidi ya watu 2,000, wakiwemo watoto. Wengi wao walishutumiwa kwa kuharibu mali ya serikali na kwa makosa ya uhaini, kosa ambalo linaweza kuadhibiwa kwa kifo chini ya sheria za nchi hiyo.
Kufuatia shinikizo kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, Ofisi ya Rais ilibuni tume huru kuchunguza vurugu zilizoshuhudiwa wakati na hata baada ya uchaguzi mkuu. Tume hiyo inatarajiwa kukamilisha ripoti yake kufikia Aprili 3.
Viongozi wa upinzani wakamatwa
Matukio kadhaa yaliripotiwa Tanzania ikiwemo kukamatwa kwa kiongozi wa chama cha upinzani cha CHADEMA Tundu Lissu na hata chama hicho kikazuiwa kushiriki kwenye uchaguzi mkuu kwa kudaiwa hakikutia saini kanuni za maadili za uchaguzi.
Sheria za kimataifa kuhusu haki za binadamu zikiwemo zile za Mkataba wa Afrika wa haki za binadamu ambao Tanzania ni mwanachama, zinaweka zuio kwa matumizi ya nguvu kupitia kiasi na maafisa wa polisi. Human Rights Watch imelalamikia ukandamizaji wa haki za raia nchini humo likitaka wahusika kuwajibishwa mara moja.