1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Tanzania inaendeleza ukandamizaji baada ya uchaguzi

5 Desemba 2025

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa Tanzania imeongeza kasi ya kuwakandamiza wapinzani wake baada ya uchaguzi wa Oktoba uliokuwa na utata na ambao ulikumbwa na vurugu kubwa.

https://p.dw.com/p/54qlI
Jeshi la polisi likiwa katika doria kwenye barabara za Dar es Salaam, Tanzania
UN yaionya Tanzania dhidi ya kuongeza kasi ya ukandamizaji baada ya uchaguzi mkuuPicha: Onsase Ochando/REUTERS

Msemaji wa ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa Seif Magango akizungumza katika kikao cha waandishi wa habari akiwa Nairobi amesema tangu katikati ya Novemba, watu kadhaa wakiwemo wasomi, maafisa wa asasi za kiraia na viongozi wa kisiasa wamekamatwa.

Baadhi wanadaiwa kukamatwa na watu wasiojulikana na ambao walikuwa na silaha. Kufikia sasa, ikiwa ni wiki tano baada ya matukio ya vurugu, mamlaka za Tanzania bado hazijatoa taarifa kuhusu idadi ya waliouawa, mazingira ya vifo hivyo wala ripoti za watu waliotoweka. "Mnamo Desemba 3, polisi ilitangaza marufuku ya jumla kwenye maandamano ya nchi nzima ya Siku Kuu ya uhuru. Tunatoa wito kwa serikali kuondoa hatua hii inayopitiliza. Tunaiomba serikali kuviagiza vikosi vya usalama kupanga na kufanya shughuli zao kwa njia ambayo itawaruhusu Watanzania kutekeleza kikamilifu haki zao za msingi."

Serikali ya Tanzania imeanzisha uchunguzi kuhusu machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi mkuu na kusababisha vifo vya watu wengi na uharibifu wa mali, ambao upinzani na waangalizi wa kigeni walidai haukuwa wa haki na usawa.