Hong Kong:Waandamanaji watawanya kwa gesi ya kutoa machozi | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.05.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

HONG KONG

Hong Kong:Waandamanaji watawanya kwa gesi ya kutoa machozi

Polisi wa jiji la Hong Kong wametumia gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha ili kuwakabili maalfu ya waandamaji waliojitokeza kupinga mswada wa sheria kali juu ya usalama wa taifa uliopendekwa na China.

Watetezi wa demokrasia katika jiji hilo wameukosoa vikali mswada huo wa sheria ambao pia unapinga kujiingiza kati kutoka nje katika mambo ya ndani ya jimbo hilo lenye mamlaka ya utawala wa ndani. Wapinzani wa sharia hiyo wanasema inaenda kinyume cha kanuni ya nchi moja mifumo miwili, inayohakikisha uhuru wa jimbo la Hong Kong usiokuwapo China bara.

Makundi ya waandamanaji waliovaa nguo nyeusi walikusanyika ili kuupinga mswada huo wa sheria. Watu hao walitoa kauli mbiu za kusisitiza msimamo wa pamoja na ukombozi wa Hong Kong. Watu wapatao 120 walikamatwa na polisi kwa kujiunga na mikusanyiko isiyoruhusiwa.

Polisi wamesema waandamanaji waliwarushia mawe na kuwapulizia unyevunyevu usiojulikana. Kwa mujibu wa taarifa ya polisi maafisa wanne walijeruhiwa. Hapo awali, mwanaharakati maarufu Tam Tak-Chi alikamatwa kwa madai ya kushiriki katika mikusanyiko isiyoruhusiwa.

Hata hivyo mwanaharati huyo amesema alikuwa anatoa nasaha juu ya masuala ya afya na kwamba alikuwa na ruhusa ya kufanya hivyo. Mswada wa sheria uliosababisha maandamano ya leo uliwasilishwa kwenye bunge la China ijumaa iliyopita na unatarajiwa kupitishwa tarehe 28 ya mwezi huu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi

Sheria hiyo itapitishwa bila ya ushiriki wa bunge la Hong Kong na utairuhusu serikali ya jiji hilo kuanzisha idara za China bara katika mji huo zitakazowawezesha maafisa wa China kuwakamata watu kiholela wataposhiriki katika harakati zitakazozingatiwa kuwa za kutetea demokrasia.

Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi amesema kuwa masuala ya Hong Kong ni ya ndani yanayo ihusu China na kwamba ujiingizaji wowote kutoka nje hautavumiliwa. Waziri Wang ameeleza kuwa ujiingizaji haramu wa kiwango kikubwa kutoka nje,katika mambo ya ndani ya Hong Kong umehatarisha sana usalama wa China.

Waziri huyo pia amehaikisha kwamba sheria inayopendekezwa haitaathiri mamlaka ya utawala wa ndani wa jiji la Hong Kong na wala haitaondoa haki na uhuru wa watu wa Hong Kong au maslahi na haki za wawekezaji vitega uchumi kutoka nje.

Hata hivyo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amesema sheria hiyo maana yake ni kuzikwa kwa mamlaka ya utawala wa ndani wa jiji hilo ambayo China iliahidi kwa kutekeleza wakati sehemu hiyo iliyokuwa koloni la Uingereza iliporejeshwa kwa China mnamo mwaka 1997. Aliyekuwa ganava wa mwisho wa Uingereza kwenye koloni hilo Chris Patten amelalamika juu ya alichokiita udikteta wa China. Amesema watu wa Hong Kong wamesalitiwa na China ambayo kwa mara nyingine imeonyesha kuwa haiwezi kuaminika.

Vyanzo:/AP/AFP