1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hofu Ujerumani juu ya ongezeko la silaha za moto kupotea

12 Februari 2026

Idadi ya silaha zinazomilikiwa binafsi na kuripotiwa kupotea au kuibiwa nchini Ujerumani imeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka minane.

https://p.dw.com/p/58YrL
Marekani | Bunduki
Silaha za moto katika maonyesho ya bunduki Las VegasPicha: Lisa Marie Pane/AP Photo/picture alliance

Hayo ni kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani ambazo zimezua mjadala mkubwa kuhusu usalama wa ndani na udhibiti wa silaha za kiraia.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, kufikia mwisho wa mwaka 2025, jumla ya silaha 47,335 zilikuwa zimesajiliwa katika daftari la kitaifa kama zilizoibwa au kupotea. Kati ya hizo, asilimia 80 — sawa na silaha 38,277 — ziliripotiwa kupotea, huku asilimia 20, yaani 9,058, zikiripotiwa kuibwa.

Hii ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na mwaka 2018, ambapo kulikuwa na silaha 24,531 ambazo hazikujulikana zilipo.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Polisi cha Ujerumani, Manuel Ostermann, amesema mwenendo huo unatia wasiwasi.

Ametahadharisha kuwa ongezeko la silaha kupotea linaweza kuashiria uwepo wa mitandao ya wahalifu wanaojihusisha na biashara haramu ya silaha, au hatari ya silaha kuangukia mikononi mwa watu wasiostahili.

Ostermann amesema, "wahalifu wasiokuwa na maadili wanaweza kutumia mianya hiyo kuongeza upatikanaji wa silaha haramu."

Licha ya changamoto hizo, Ujerumani bado ina idadi kubwa ya silaha zinazomilikiwa kisheria. Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa hadi mwisho wa Desemba, kulikuwa na takriban silaha za moto milioni tano zinazomilikiwa na wawindaji, washiriki wa michezo ya kulenga shabaha na wakusanyaji wa silaha. Aidha, zaidi ya vipuri 526,000 vya silaha vilikuwa vimesajiliwa.