Hatua ya Saakashvili ni kamari itakayogharimu sana nchi yake | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 12.08.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

IDHAA YA KISWAHILI

Hatua ya Saakashvili ni kamari itakayogharimu sana nchi yake

Matumaini ya Georgia ya kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi NATO na Umoja wa Ulaya yamepata pigo kwa sababu ya mapigano ya wiki hii na Urusi na hiyo kupunguza vivutio vyake kwa wawekezaji.

default

Rais Mikheil Saakashvili wa Georgia.

Hatua ya Rais Mikeil Saakashvili kutuma vikosi Ossetia Kusini inaonekana kuwa kama kamari ambayo itaigharimu sana nchi yake ya Georgia.

Mzozo juu ya jimbo lililojitenga la Ossetia Kusini umeibuwa upya tafauti zilioko kati ya Marekani na Ulaya na ndani ya Ulaya yenyewe juu ya Georgia na kudhoofisha zaidi imani ya baadhi ya nchi kwa kiongozi wake anayeungwa mkono na Marekani.

Ni miezi minne tu iliopita Rais Mikheil Saakashvili alikuwa akipongeza mafanikio aliyopata katika harakati zake za kujiunga na mataifa ya magharibi wakati viongozi wa Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi NATO walipotangaza katika mkutano wao wa viongozi kwamba Georgia na nchi mwenzake ya Ukraine iliokuwa ikiunda muungano wa Urusi wa zamani iko siku zitajiunga na jumuiya hiyo.

Hata hivyo nchi kadhaa za Ulaya ya magharibi ikiwemo Ujerumani zimekuwa na mashaka kuhusu kutanuwa mkataba huo wa kijeshi unaongozwa na Marekani hadi kufikia mipaka ya kusini mwa Urusi na kuhusu utulivu wa Georgia kutokana na matatizo yake na majimbo mawili yanayotaka kujitenga.

Zimeizuwiya NATO kuzipa nchi hizo Mpango wa Uwanachama wa Utekelezaji ambao ni mpango hatimae unaopelekea kupata uwanachama. Mawaziri wa mambo ya nje wa jumuiya hiyo wanatarajiwa kulichambuwa tena suala hilo mwezi wa Desemba.

Uamuzi wa Saakashvili kutuma vikosi huko Ossetia Kusini mojawapo ya maeneo ya waasi kumeifanya Urusi iingile kati kijeshi na mapambano ukingoni mwa jimbo jengine linalotaka kujitenga la Abkhazia yamezidi kuongeza wasi wasi huo.

Waziri wa mambo ya nje wa Italia amesema kwenye mahojiano na gazeti yaliochapishwa Jumatatu kwamba vita hivyo vimeitenga zaidi Georgia sio tu na Ulaya bali pia kufanya mkutano wa NATO hapo mwezi wa Desemba kuwa mgumu.

Ameliambia gazeti la La Stampa kwamba Italia inashikilia kwamba hawawezi kuanzisha muungano dhidi ya Urusi barani Ulaya na katika kipengele hicho wako karibu na msimamo wa Waziri Mkuu wa Urusi Vladimir Putin.

Georgia imepata ukuaji uchumi wa kuvutia na imevutia mtaji wa kigeni licha ya vikwazo vya kiuchumi na uchukuzi vya Urusi pamoja na kukatiwa gesi kwani kiu ya wawekezaji kwa Ulaya inayoinukia inaelekea mashariki kwa kiasi fulani kutokana na matumaini ya nchi hiyo kuwa nanga ya miundo ya usalama kati ya Ulaya na Marekani.

Ujerumani na Ufaransa ambazo zote zina ushirikiano wa karibu na Urusi zimekuwa na hadhari katika matamshi yao ya hadharani zikitowa wito wa kusitishwa kwa mapigano haraka na kuheshimiwa kwa mipaka ya Georgia lakini zikijiepusha kulaumu upande wowote ule kwa kuanzisha mapigano hayo.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani amesema Kansela Angela Merkel ataendelea na mpango wake kwenda Sochi katika mwambao wa bahari Nyeusi nchini Urusi hapo Ijumaa kwa mazungumzo na Rais Dmitry Medvedev.

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ambaye anashikilia Urais wa Umoja wa Ulaya leo anatembelea Urusi na Georgia kwa matarajio ya kuleta suluhu.

Uingereza imelani mashambulizi ya Urusi ndani ya Georgia na mataifa ya zamani ya kikomunisti ya Baltik pamoja na Poland yameishutumu Urusi kwa uchokozi na ubeberu.

Pengine matamshi yalio makali kabisa ya Ulaya yametolewa na waziri wa mambo ya nje wa Sweden Carl Bildt ambaye amesema kwamba madai ya Urusi kwamba inawalinda raia wake huko Ossetia Kusini yanamkumbusha mbabe wa Serbia Slobodan Milosevic na dikteta wa Manazi Adolf Hitler.

Wanadiplomasia wanasema kwamba kwa kadri Urusi haitochukua hatua zake za kijeshi kupindukia na kutotishia bomba muhimu la mafuta huko Bahari Caspian linaloelekea Uturuki kupitia Georgia au kutaka kumpinduwa Saakashvili hakuna matarajio ya kuchukuliwa kwa hatua kali ya pamoja na mataifa ya magharibi.

Kuna wanadiplomasia wanaoshukuru kwamba Georgia haikuwa mwanachama wa NATO venginevyo ingeliweza kutumia kifungu nambari tano cha ulinzi wa pamoja ambacho nchi wanachama zinatakiwa kutowa msaada wakati mwanachama mwenzao anaposhambuliwa.

 • Tarehe 12.08.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EvI2
 • Tarehe 12.08.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EvI2
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com