Hariri akiri chama chake kimepoteza viti kwenye uchaguzi huu | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Lebanon

Hariri akiri chama chake kimepoteza viti kwenye uchaguzi huu

Katika uchaguzi wa bunge wa nchini Lebanon chama cha Mustakabal cha waziri mkuu Saad al Hariri kinachoungwa mkono na nchi za Magharibi kimepoteza viti vingi katika ngome yake kuu ya kisiasa mjini Beirut.

Kwa jumla Waziri Mkuu wa Lebanon Saad al Hariri amesema chama chake cha Mustakabal kimepoteza theluthi moja ya viti katika uchaguzi huo wa bunge kwa kupata viti 21 ikilinganishwa na idadi ya viti 33 katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2009.

Waziri mkuu wa Lebanon Saad al Hariri (picture-alliance/AP/dpa/H. Malla)

Waziri mkuu wa Lebanon Saad al Hariri

Waziri huyo mkuu wa Lebanon amesema chama chake kilikuwa na matumaini ya kufikia matokeo bora lakini amesema hata hivyo chama hicho kilikabiliwa na upinzani mkali uliokuwa na lengo la kukiondoa chama hicho kwenye medani za kisiasa. Hariri pia amelaumu sheria mpya za uchaguzi. Wakati huo huo waziri mkuu huyo wa Lebanon Saad al Hariri ameitaka jumuiya ya kimataifa kuyapokea matokeo ya uchaguzi wa Lebanon kwa njia nzuri.

Lebanon ilikuwa na uchaguzi wake wa kwanza wa bunge tangu 2009 hapo jana Jumapili. Nchi hiyo inataka kuithibitishia jumuiya ya kimataifa ikiwa ni pamoja na wafadhili na wawekezaji ambao mwezi uliopita waliahidi zaidi ya dola bilioni 11 kwa ajili ya kuisaidia Lebanon. Nchi hiyo inataka kuthibitisha kwamba ina mipango ya kuaminika ya kurekebisha uchumi wake na kufanya uchaguzi ilikuwa ni sehemu mojawapo muhimu.

Kiongozi wa kundi la Hezbollah nchini Lebanon Hassan Nasrallah (picture-alliance/dpa)

Kiongozi wa kundi la Hezbollah nchini Lebanon Hassan Nasrallah

Lakini ikiwa matokeo ya awali yatathibitishwa kundi la Hezbollah na washirika wake wa kisiasa watapata msukumo mkubwa nchini Lebanon na pia katika nchi jirani ya Syria ambako Hezbollah imezidi kuimarisha ushawishi wake mnamo miaka ya hivi karibuni. Juu ya matokeo hayo mchambuzi wa masuala ya siasa kwenye gazeti la Al-Nahar bwana Ibrahim Bayram ameeleza kwamba matokeo hayo, kimsingi si ya kushangaza kutokana na uchunguzi wa maoni uliofanywa kabla ya uchaguzi. Vyama vya kizalendo vimeimarika wakati chama cha Mustakabal cha waziri mkuu Hariri kimepoteza umaarufu. Pamoja na hayo Hezbollah na washirika wake wamepata mafanikiojapo hilo lilitazamiwa. Sasa wanao wajumbe zaidi ya 50.

Rais Michel Aoun na waziri mkuu Hariri wamepoteza baadhi ya viti lakini bado wana mfungamano mkubwa kabisa wa Wakristo na Waislamu wa madhehebu ya Sunni. Chama cha rais Auon cha Free Patriotic Movement sasa kina viti 21 yaani pungufu ya viti sita vya hapo awali. Chama cha waziri mkuu Hariri kitakuwa na wabunge 20 Hapo awali chama hicho kilikuwa na wabunge 32. Angalau mjumbe mmoja mwanamke amepata kiti cha bunge kwa tiketi ya asasi ya kijamii.

Uchaguzi wa jana ulishuhudia ushiriki wa kiwango cha chini cha  wapiga kura. Kwa mujibu wa  taarifa ni asilimia 49.2 tu ya wapiga kura walioshiriki. Serikali ijayo ya Lebanon itakuwa ya umoja kama ile inayoondoka sasa itakayowajumuisha Hezbollah mahasimu wa waziri mkuu Hariri.

Bango lenye picha za Waziri mkuu wa Lebanon Saad Hariri na kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah (Reuters/A. Taher)

Bango lenye picha za Waziri mkuu wa Lebanon Saad Hariri na kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah

Matokeo rasmi yatangazwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Nouhad Machnouk baadaye leo ingawa haijulikani hasa ni muda gani.Katika uchaguzi huo wa bunge ambao ni wa kwanza kufanyika baada ya takriban muda wa mwongo mmoja, nchini  Lebanon, chama cha Hezbollah na washirika wake wa kisiasa wanatarajiwa kupata  viti visivyopungua 47 katika bunge lenye jumla ya viti 128. Kutokana na wingi huo wa viti kundi la  Hezbollah na washirika wake wa kisiasa wataweza kuwa na kura ya turufu bungeni na kuzuia kupitishwa sheria yoyote wanayoipinga.

Mwandishi: Zaianab Aziz/APE/AFPE/RTRE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

 

 

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com