Guinea yakumbuka mauaji ya 2009 | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.09.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Guinea yakumbuka mauaji ya 2009

Leo (28.09.2011) ni miaka miwili kamili tangu jeshi la Guinea lilipowavamia waandamanaji katika uwnaja wa mpira mjini Conakry na kuwauawa zaidi ya 100 katika tukio linalotajwa kama mauaji ya maangamizi.

Rais Alpha Conde wa Guinea

Rais Alpha Conde wa Guinea

Kiasi ya watu 50,000 walikusanyika kwenye uwanja wa michezo tarehe 28 Septemba 2009. Walitaka kuandamana kwa amani dhidi ya utawala wa kijeshi wa Guinea ambao ulikuwa umekaa madarakani kwa mwaka mmoja tangu kuupindua utawala wa kidikteta.

Lakini muda mchache kabla ya maandamano kuanza, vikosi vya kijeshi na vya usalama viliingia kwenye uwanja huo na vifaru vya kivita na silaha za moto na kuanza kuwamwagia risasi waandamanaji.

Bwawa la damu ndiyo yaliyokuwa matokeo yake, kwani watu zaidi ya 150 waliuawa, wengine zaidi ya 1200 walijeruhiwa na watoto 100 wakaacha mayatima.

Mhusika mkuu wa mauaji haya alikuwa ni kiongozi wa kijeshi, Moussa Dadis Camara, ambaye naye alikuwa ameingia madarakani kupitia mapinduzi. Baada ya kumuondosha madarakani Rais Lansana Conte, Camara mwenyewe alianza kutawala kwa mkono wa chuma. Watu walitaka kuandamana kupinga utawala huu na walitaka ukatili ukome, lakini walichokipata ni kile walichokipinga.

Machafuko ya mwaka 2010 nchini Guinea

Machafuko ya mwaka 2010 nchini Guinea

Mariame Sy alikuwa mmoja wa waandamanaji hao, na hadi leo ameshindwa kuusahau mkasa wenyewe ulivyotokea.

"Nilikuwa uwanjani, kwenye eneo walilokaa wanawake. Mara tu baada ya kufika, mwanajeshi mmoja akanipiga kwa nguvu. Nilimuona vyema alivyokuwa akinifanya. Nilishituka sana, niliumia sana. Ilikuwa kama ndoto. Kila siku nilifikiria kuwa kuna siku ningelikuwa muhanga mwengine." Anasema Mariame.

Lakini ni baada ya mauaji haya, ndipo mambo yalipoanza kufunguka nchini Guinea: kukafanyika jaribio la mauaji dhidi ya Moussa Dadis Camara, na aliyehusika ni mtu wake wa karibu, Aboubakar Diakite.

Matokeo yake, Camara alijeruhiwa vibaya na kupelekwa matibabuni nje ya nchi na makamo wake, Jenerali Sekouba Konate, akakaimu wadhifa wake akiahidi kuirudisha Guinea katika utawala wa kidemokrasia.

Chini ya Jenerali Konate, Novemba 2010 uchaguzi ulifanyika na mgombea wa upinzani, Alpha Conde, akachaguliwa kuwa rais wa kwanza wa kidemokrasia tangu taifa hilo lipate uhuru mwaka Oktoba 1958.

Hali iliyopo nchini Guinea hivi sasa, ikiwa ni miaka miwili tangu mauaji yafanyike na karibuni mwaka mmoja tangu uchaguzi wa rais, inachukuliwa kuwa ni nzuri na watu wengi.

Mwanamme mmoja mjini Conakry amesema kwamba mambo mengi yamebadilika, kuanzia na hili la kuwa sasa Guinea inaongozwa na rais aliyechaguliwa kidemokrasia. "Naamini kwamba ana dhamira ya kubadilisha mambo mengi. Na naamini sisi raia tunapaswa kumsaidia kutimiza dhamira hii."

Lakini mwengine anadhani kuwa katika kiwango cha maisha ya mtu wa kawaida, hakuna kilichobadilika. "Lakini kwa nje bila ya shaka tunaongozwa na serikali ya kidemokrasia, na wanajeshi sasa hawapo tena madarakani."

Lakini demokrasia hii changa ya Guinea ina safari refu ya kwenda. Hadi sasa uchaguzi wa Bunge haujafanyika, na kuna mengi ya kufanywa ili kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa nao wa kidemokrasia, hapo utakapofanyika Disemba 29.

Vyama vya upinzani vinalalamikia tarehe hii, kwa hoja kuwa Tume ya Uchaguzi na serikali hazikuvishirikisha kwenye mchakato wa uchaguzi, ikiwemo hatua ya usajili wapiga kura, ambayo wapinzani wanasema imeshaghushiwa na serikali.

Mwandishi: Dirke Köpp/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Othman Miraji

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com