Guinea: Mwaka mmoja wapita bila ya wauaji kukamatwa | Habari za Ulimwengu | DW | 28.09.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Habari za Ulimwengu

Guinea: Mwaka mmoja wapita bila ya wauaji kukamatwa

Mwaka mmoja baada ya mauaji ya kuangamiza yaliyofanywa na vikosi vya jeshi la Guinea mjini Conakry, hakuna hata afisa mmoja kati ya wanaoshukiwa kuhusika na mauaji hayo aliyefikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kiongozi wa Serikali ya Muda ya Guinea, Jenerali Sekouba Konate, akipiga kura katika uchaguzi wa Juni 27, 2010.

Kiongozi wa Serikali ya Muda ya Guinea, Jenerali Sekouba Konate, akipiga kura katika uchaguzi wa Juni 27, 2010.

Siku kama ya leo, tarehe 28 Septemba mwaka 2009, vikosi vya jeshi la Guinea viliyasambaratisha kinyama maandamano yaliyoandaliwa na upinzani katika viwanja vya michezo mjini Conakry. Watu 157 waliuawa, mamia ya wanawake wakabakwa na maelfu wakajeruhiwa.

Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Kimaitaifa ya Uhalifu (ICC) wanasema kilichotokezea siku hiyo ni uhalifu dhidi ya ubinaadamu. Lakini ripoti iliyochapishwa Jumatatu ya wiki hii na Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binaadamu (FIDH) na Jumuiya ya Kutetea Haki ya Binaadamu ya Guinea (OGDH), inaelezea kukwama kabisa kwa hatua ya kisheria dhidi ya waliohusika na uhalifu huo.

Ibrahim Barry, mmoja kati ya watu waliokuwapo kwenye maandamano hayo, anasema kwamba haoini ikiwa kuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi ya wauaji, licha ya kuwepo kwa ushahidi wa kutosha.

Mkasa wa mauaji haya unaelezea namna vikosi vya jeshi vilivyoingia kwenye uwanja huo wa michezo, vilivyomimina risasi kwa watu, vilivyobaka wanawake wa kila umri na vilivyowapiga mashahidi na viongozi wa upinzani.

Mmoja wa wanawake waliopatwa na mkasa huo, Salematou Bangoura, ameliambia Shirikia la Habari la AFP, kwamba hakumbuki ni wanaume wangapi waliombaka, kwa sababu alipoteza fahamu wakati akitendewa unyama huo, lakini anakumbuka kwamba alichukuliwa kwenye jumba la mwanajeshi mmoja alikofungiwa huku akibakwa kwa siku nne mfululizo.

Kwa mujibu wa FIDH, hapo awali utawala wa kijeshi ulikusudia kulinyamazisha suala hili kwa kuunda tume yake yenyewe ya uchunguzi, ambayo iliongozwa na Aboubakar Sidiki Diakite, aliyekuwa mtu wa karibu wa kiongozi wa kijeshi Moussa Dadis Kamara.

Lakini kwa miezi kumi sasa, Diakite mwenyewe amekimbilia mafichoni baada ya kushindwa kwa jaribio lake la kumuua Camara kwa risasi, miezi miwili baada ya mauaji hayo ya maangamizi. Diakate anadai kwamba alilazimika kumpiga risasi Camara kwa kuwa serikali ilimbebesha yeye Diakite jukumu lote la sakata ya mauaji.

Baada ya kunusurika kifo, mwezi Januari mwaka huu, Camara alihamia nchini Burkina Faso na nafasi yake ikachukuliwa na Jenerali Sekouba Konate ambaye anasimamia serikali ya mpito kuelekea uchaguzi wa rais.

Kutokana na shinikizo la Jumuiya ya Kimataifa na mahakama ya ICC, hatimaye majaji watatu waliteuliwa katika mwezi wa Februari mwaka huu, kuchunguza mauaji hayo ya maangamizi. Lakini hadi sasa ni wanajeshi wawili tu wa ngazi ya chini ndio waliokamatwa, huku wale hasa walioamuru kufanyika kwa mauaji haya, yaani wanajeshi wa ngazi za juu na wanasiasa, wakiwa bado hawajaguswa kabisa na mfumo wa kisheria wa Guinea.

Tume ya uchunguzi iliyoteuliwa na Umoja wa Mataifa inasema kwamba Camara ana dhamana ya moja kwa moja ya uhalifu huo, kwani yeye ndiye aliyekuwa amiri jeshi mkuu mauaji yalipofanyika.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com