Ghana-Uchaguzi waingia awamu ya mwisho | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 02.01.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IDHAA YA KISWAHILI

Ghana-Uchaguzi waingia awamu ya mwisho

Uchaguzi nchini Ghana waingia awamu ya mwisho na muhimu kabisa kuamua nani atakayoliongoza taifa hilo baada ya rais wa sasa John Kufuor kukamilisha kipindi chake cha uongozi tarehe 7 mwezi huu.

Wapiga kura wakisubiri kupiga kura zao kumchagua rais mpya nchini Ghana.

Wapiga kura wakisubiri kupiga kura zao kumchagua rais mpya nchini Ghana.


Zaidi ya wapiga 53,000 waliojiandikisha katika eneo bunge la Tain, eneo ambalo halikushiriki uchaguzi wa siku ya jumapili, walijitokeza kupiga kura kuamua mshindi wa duru ya pili ya uchaguzi huo, licha ya wito kutolewa na chama tawala cha New Patriotic kinachoongozwa na Nana Akufo Addo, kuwataka wafuasi wake kususia uchaguzi huo.


Hadi kufikia sasa kiongozi wa chama cha upinzani cha Nationa Democratic Congress NDC, John Atta Mills anaongoza kwa zaidi ya kura 23,000 dhidi ya mpinzani wake Akufuor Addo.


Uchaguzi katika eneo bunge hilo la Tain lenye uwezo mkubwa wa shughuli za kilimo uliendelea baada ya wakaazi wa eneo hilo kukosa fursa hiyo ya kupiga kura siku ya Jumapili, kutokana na dosari zilizotokea katika usafirishaji wa makaratasi ya kupigia kura.

Shughuli hiyo iliendelea licha ya chama tawala cha New Patriotic NPP, kwenda mahakamani kutaka uchaguzi huo usimamishwe kwa kile ilichodai kuwa mazingira yasiyofaa katika eneo hilo kuendesha uchaguzi wa huru na haki.


Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa chama hicho kwenda mahakamani kupinga shughuli hiyo ya uchaguzi, baada ya juhudi za awali kutaka kuizuia tume ya uchaguzi nchini humo kutangaza matokeo ya uchaguzi huo, kwa madai ya visa vya udanganyifu katika maeneo yenye ufuasi mkubwa wa chama cha upinzani.


Hata hivyo mahakama iliamuru kesi hiyo isikizwe siku ya Jumatatu na kukitaka chama cha NPP kuwasilisha maagizo hayo kwa tume ya uchaguzi na vile vile kwa chama cha NDC kabla ya kusikizwa kwa kesi hiyo Jumatatu ijayo. Matokeo kamili ya uchaguzi pia yanatarajiwa siku hiyo ya jumatatu.


Ripoti zinaeleza kuwa mawakala wa chama tawala cha NPP, walikuwa wakizunguka usiku wa kuamukia Ijumaa katika miji na vijiji vya eneo bunge hilo, wakitumia vipaza sauti kuwataka wakaazi wa eneo hilo kususia uchaguzi huo, hali iliyokonekana kinyume kabisa na shughuli ilivyoendelea ambapo wapiga kura walijitokeza kwa wingi kupiga kura zao bila ya visa vyovyote viliyoripotiwa.


Maafisa wa uchunguzi wanasema kuwa waakilishi wa chama cha upinzani cha NDC waliofika mapema katika vituo vya kupigia kura kushuhudia shughuli hiyo ikianza,lakini waakilishi wa chama tawala hawakuonekana katika baadhi ya vituo hivyo.


Matokeo ya mapema ya uchaguzi wa siku ya Jumapili kutoka maeneo bunge 299,yanaonyesha kuwa John Atta Mills anaongoza kwa asilimia 50.13 dhidi ya kiongozi wa chama tawala John Akufour aliya na jumla ya asilimia 49.87.


Hali ya usalama imeimarishwa katika eneo hilo lenye uwezo mkubwa wa kuzalisha zao la Kakao,baada ya jeshi na maafisa wa usalama wa taifa kupelekwa kudumisha amani, ili kuzuia uwezekano wa kutokea vurugu la baada ya uchaguzi kama ilivyoshuhudiwa mwaka uliopita nchini Kenya na Zimbabwe.


Vyama hivyo viwili vimekuwa vikilaumiana kwa visa vya udanganyifu na ghasia zilizoshuhudiwa siku ya Jumapili.

Rais John Kufuor ambaye ameponmgezwa kwa hatua yake ya kungatuka madarakani baada ya kukamilisha vipindi vyake viwili vya utawala, amezitaka pande hizo mbili kuheshimu matokeo ya uchaguzi huo.


Kiongozi wa upinzani John Atta Mills yadaiwa anaungwa mkono na wengi katika eneo bunge hilo la Tain, na wadadisi wanasema kuwa huenda akashinda uchaguzi huu ambao ni wa tano kuandaliwa kidemokrasia tangu mwaka wa 1992.


Mashirika na mataifa mbali mbali yamepeleka wachunguzi wake kwenye uchaguzi wa leo, ikiwa ni pmaoja na mataifa ya Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Africa Magharibi ECOWAS.

Uchaguzi wa taifa hilo lililojipatia uhuru mwaka wa 1957 wake kutoka kwa Uingereza, unachukuliwa kuwa mtihani mkubwa wa demokrasia katika bara la Africa, ambalo limeshuhudia ghasia za umwagikaji wa damu kutokana na mng`anganio wa uongozi.


Chama cha New Patriotic cha John Akufuor kilishinda duru ya kwanza ya uchaguzi uliofanyika tarehe 7 mwezi Disemba mwaka uliopita, ingawa hakikupata ushindi wa moja kwa moja kukiwezesha kuunda serikali.


Wakati wa duru ya kwanza ya uchaguzi huo chama cha NDC kilipata jumla ya Viti 114 dhidi ya viti 107 vilivyonyakuliwa na chama cha NPP, hali iliyopelekea duru kuandaliwa kwa duru ya pili ya uchaguzi.

 • Tarehe 02.01.2009
 • Mwandishi Eric Kalume Ponda
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GQvo
 • Tarehe 02.01.2009
 • Mwandishi Eric Kalume Ponda
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GQvo
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com