Fahari iliyomo kwenye Nishani ya Nobel | Habari za Ulimwengu | DW | 07.10.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Habari za Ulimwengu

Fahari iliyomo kwenye Nishani ya Nobel

Ni mara chache kwa mji wa Oslo kusikika kwenye vyombo vya habari ulimwenguni, lakini angalau mara mbili kwa mwaka, Nishani ya Amani ya Nobel huufanya mji huo mkuu wa Norway utupiwe macho na ulimwengu mzima.

Mshindi wa mwaka 2010 wa Nishani ya Amani ya Nobel katika Fasihi, Mario Vargas Llosa wa Peru

Mshindi wa mwaka 2010 wa Nishani ya Amani ya Nobel katika Fasihi, Mario Vargas Llosa wa Peru

Tarehe 10 Disemba mwaka 1901 katika Baraza la Manispaa la Oslo, tunzo ya kwanza ya Amani ya Nobel ilitolewa kwa watu wawili: Henri Dunant, ambaye ndiye mwanzilishi wa Chama cha Msalaba Mwekundu na Frederic Passy, mwanzilishi wa chama cha kwanza cha kupigania amani nchini Ufaransa.

Hili lilikuwa ni tukio la kwanza la kutimiza usia wa Alfred Nobel, ambaye mwaka mmoja kabla ya kifo chake, aliusia asilimia 94 ya mali yake itumike kwa ajili ya kuwatunza watu watakaochangia katika amani na maendeleo ya wanaadamu wenzao. Wakati anafariki, mwezi Novemba mwaka 1895, utajiri wa Alfred Nobel ulikuwa unakaribia dola milioni 200 za Kimarekani.

Medali ya Nishani ya Amani ya Nobel

Medali ya Nishani ya Amani ya Nobel

Kutoka mwaka 1901 hadi sasa, watu 100 na jumuiya 20 zimeshapata heshima hii ya kupokea nishani ya Nobel, ambapo sio tu kwamba hupewa medali za dhahabu, bali pia stashahada rasmi za kutambua mchango wao, pamoja na pesa taslim, Euro milioni moja.

Alfred Nobel hakuusia namna tu ya kuzigawa tunzo hizi, bali pia namna ambavyo majaji wangewachagua washindi wa tunzo zenyewe. Kuna kamati tano za uteuzi, ambamo ndani yake muna wajumbe kutoka bunge la Norway, na ujumbe katika kamati hizi hudumu kwa kipindi cha miaka sita. Kamati inatakiwa iwe huru na isiyoathiriwa na mitazamo yoyote ile. Vikao vya kamati hii vinakuwa havina itifaki, na vinaweza kukaa wakati wowote lakini maamuzi yake lazima yapitishwe na idadi kubwa ya wajumbe.

Katika mwaka huu wa 2010, Kamati ya Nobel ilipokea mapendekezo 237. Kabla ya mapendekezo kupitishwa, hupimwa na watu na taasisi mbalimbali, kama vile washindi wa zamani wa tunzo hii, serikali, Mahakama ya Kimataifa ya The Hague, viongozi wa taasisi za utafiti, jumuiya na au maprofesa wa vyuo vikuu vinavyohusika na fani inayotolewa tunzo. Baada ya hapo, mwanzoni mwa mwezi wa Februari, Kamati ya Nobel hukutana kuchagua majina 20 ya wagombeaji tunzo hiyo, na kisha wataalamu wa fani husika, huwaandikia wagombea walioteuliwa. Hadi katikati ya Septemba, Kamati ya Nobel inatakiwa iwe tayari imeshafanya maamuzi, sio tu kuhusu nani anapokea tunzo, bali pia kuhusu sheria za tunzo hiyo.

Mwanzoni tunzo hii ilikuwa inakwenda kwa wawakilishi wa jumuiya zinazojihusisha na mambo ya amani. Baadaye ikaanza kwenda pia kwa watu wanaojihusisha na mambo ya kibinaadamu na utafutaji amani kwa njia za kidiplomasia, hasa katika mazingira ambapo milango ya amani imeonekana kufungwa kabisa. hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa tunzo ya mwaka 1994, ambayo ilikwenda kwa Shimon Perez, Yitzhak Rabin na Yassir Arafat kutokana na mchango wao katika kutafuta suluhu ya mgogoro wa Mashariki ya Kati. Hivi sasa, tunzo hii inakwenda hata kwa watu wanaopigania haki za binaadamu na ulinzi wa mazingira duniani.

Tarehe 10 Disemba, ambayo ni sawa na siku aliyofariki Alfred Nobel, katika hadhara ya mfalme wa Norway, kwenye jengo la Manispaa ya Oslo, tunzo hii ndipo inapotolewa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Mathias von Hein/ZPR

Mpitiaji: Charo, Josephat

DW inapendekeza

 • Tarehe 07.10.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PYlA
 • Tarehe 07.10.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PYlA
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com