1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
AfyaChina

EU yachukua hatua kufuatia mlipuko wa UVIKO-19, China

5 Januari 2023

Umoja wa Ulaya umeyahimiza mataifa wanachama kuweka kanuni ya kufanywa vipimo kabla ya safari, kwa abiria wote kutoka China- katika wakati taifa hilo linakabiliwa na ongezeko la maambukizi ya UVIKO-19.

https://p.dw.com/p/4Ll6D
China Covid-19 | Kontrollen beim Flughafen in Madrid
Picha: Alberto Ortega/Europa Press/abaca/picture alliance

Maambukizi ya UVIKO-19 yameongezeka nchini China hasa katika mji mkuu Beijing. Wanaoathirika zaidi ni wazee. Hospitali ya Chuiyangliu iliyopo mashariki mwa jiji hilo imeshuhudia uhaba wa vitanda vya kuwalaza wagonjwa kutokana na idadi kubwa ya maambukizi.

China Covid-19 | Patienten in Shanghai
Wagonjwa wa UVIKO-19 katika Hospitali ya mjini Shanghai, China-Januari 03,2023Picha: Ray Young/Utuku/ROPI/picture alliance

Ongezeko la wagonjwa mahututi wanaohitaji huduma ya hospitali inajiri baada ya China kuachana mwezi uliopita na hatua yake ya vizuizi vikali vya kukabiliana na janga hili la UVIKO-19, hatua ambazo ziliuelemea uchumi wa taifa hilo na kusababisha maandamano makubwa kuwahi kushuhudiwa tangu mwishoni mwa miaka ya 1980.

Soma zaidi:Ulaya na mkakati wa kuwapima UVIKO-19 abiria kutoka China 

EU-Gipfel in Brüssel | Bundeskanzler Olaf Scholz und Präsident Macron
Waliombele: Kushoto: Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Kulia: Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wakiwa mjini Brussels, UbelgijiPicha: John Thys/AP Photo/picture alliance

Jana, viongozi wa Umoja wa Ulaya waliokutana mjini Brussels nchini Ubelgiji, waliyahimiza mataifa wanachama kuweka kanuni ya kufanywa vipimo vya UVIKO-19 kabla ya safari, kwa abiria wote kutoka China. Hatua hiyo ambayo tayari imekosolewa na mashirika ya ndege, huenda ikaikasirisha Beijing.

Hata hivyo Umoja wa Ulaya haikuafikiana kwamba mataifa yote 27 wanachama yaweke kanuni ya aina hiyo ambayo nchi kama Italia, Ufaransa na Uhispania zilikuwa tayari zinaitekeleza katika ngazi ya kitaifa.

China yapinga hatua hiyo

China tayari imepinga vikali hatua za aina hiyo, ikionya kulipiza kisasi kama sera hiyo itaamuliwa kote katika jumuiya hiyo.

WHO Generaldirektor Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni WHO, Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: Fabrice Coffrini/KEYSTONE/picture alliance

Aidha, Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema jana kuwa ana wasiwasi juu ya ukosefu wa data ya mlipuko wa UVIKO-19 kutoka serikali ya China. Shirika hilo limebaini kuwa kufikia Januari 01, 2023, China iliripoti visa vipya vya maambukizi 218,019 na vifo 648.

Soma zaidi: China yakosoa vizuizi vya UVIKO dhidi ya raia wake

Leo Alhamisi, China imesisitiza kwamba imekuwa wazi kwa jamii ya kimataifa juu ya takwimu zake za UVIKO-19 na imetoa wito kwa Shirika la Afya Ulimwenguni  kuchukua msimamo "wa haki" juu ya suala hilo.

Frankreich Lyon | Coronavirus Impfstation
Muuguzi akitayarisha chanjo ya UVIKO-19 ya Pfizer-BioNTech Picha: JEFF PACHOUD/AFP

Wakati huohuo, Wajerumani wanaoishi China wameanza hii leo kupatiwa chanjo ya UVIKO-19 ya BioNTech. Hili ni tukio la kwanza la utoaji wa chanjo ya kigeni katika nchi hiyo ambayo haijaidhinisha matumizi ya chanjo zisizo za Kichina licha ya maambukizi kuongezeka.

Hii ni kutokana na makubaliano yaliyofikiwa mwezi Novemba wakati wa ziara ya Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz mjini Beijing. Wajerumani wenye umri wa miaka 12 na zaidi wanaweza kupokea dozi yao ya kwanza au ya ziada katika hospitali teule ya kimataifa katika miji ya Beijing, Shanghai, Shenyang, Guangzhou au Chengdu.