Ethiopia yapitisha sheria ya kupinga ugaidi | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.07.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ethiopia yapitisha sheria ya kupinga ugaidi

Sheria hiyo imepitishwa na serikali ya chama cha EPRDF

default

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi


Kiasi cha miaka 18 iliyopita wakati utawala wa chama cha Ethiopian Peoples Revolutionary Democratic Front (EPRDF)cha nchini humo kilipochukua madaraka, watu walikuwa na hamu ya kuwa na demokrasia ambayo hata watoto walianza kubishana na wazazi wao, wakisema hii ni haki yangu ya kidemokrasia.

Mwanzoni mwa mwezi huu, sheria mpya ya kupinga ugaidi imeanzishwa nchini Ethiopia, ikitoa idhini kwa kuipa mamlaka taifa hilo kuwakamata watu wanaodhaniwa kuwa ni tishio. Sheria hiyo inafanana kwa karibu kabisa na ile inayoyazuia shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali NGO's hasa yale yanayotetea haki za binaadamu. Wakati miaka 17 ya mapambano ya silaha yalipouondoa madarakani utawala wa kidikteta wa Mangistu Haile Mariam mwaka 1991, chama cha EPRDF kilianza kuzungumzia kuhusu demokrasia, usawa na haki za binaadamu.

Mwezi Januari mwaka 1993, serikali ya Ethiopia ilichukua hatua kali za kikatili dhidi ya wanachuo wa Chuo Kikuu cha Addis Ababa (AAU), waliokuwa wanapinga kura ya maoni kuhusu uhuru wa Eritrea. Hatua hiyo ilisababisha kifo cha mwanachuo mmoja na wengine 85 kujeruhiwa. Mwezi Aprili, mwaka huo huo wa 1993, serikali iliwafukuza kazi maprofesa 40 wa chuo hicho Kikuu cha Addis Ababa, kutokana na maprofesa hao kuwa wakosoaji wakubwa wa serikali.

Baada ya hapo lilifuata sakata la Chama cha Waalimu wa Ethiopia (ETA), ambapo viongozi wake walifungwa. Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch linalituhumu Jeshi la Polisi nchini humo kumuua kwa kumpiga risasi kaimu mkurugenzi wa chama hicho cha ETA, Assefa Maru, mwaka 1997.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2005, vyama vya upinzani nchini humo havikufanikiwa kupata nafasi kubwa katika vyombo vya habari vya serikali. Upinzani ulishinda viti kadhaa vya bunge, lakini serikali ilinyamazisha baadhi ya maeneo, hivyo upinzani haukufanikiwa katika maeneo hayo. Hatua hiyo ilisababisha maandamano katika mitaa ya Addis Ababa, yaliyopelekea vifo vya karibu watu 200 vilivyotokana na vikosi vya usalama.

Bunge la Ethiopia sasa limepitisha sheria hiyo ya kupinga ugaidi, ambayo awali ilipendekezwa na Usalama wa taifa na wataalamu katika Wizara ya Sheria miaka minne baadaye, na hatimaye kupitishwa na Baraza la Mawaziri mwanzoni mwa mwezi uliopita. Sheria hiyo mpya ya Ethiopia, inaueleza ugaidi kama njia inayohusisha vitendo visivyosababisha vurugu au majeraha kwa watu kama vile makosa ya jinai na kuingilia shughuli za umma. Adhabu ya kosa hilo ni kifungo cha miaka 15 jela hadi maisha au hata hukumu ya kifo. Sheria hiyo pia inawapa polisi mamlaka ya kukamata na kufanya upekuzi bila dhamana ya shughuli hiyo.

Beyene Petros, mwenyekiti wa chama cha upinzani cha United Ethiopian Democratic Forces kilichoipinga sheria hiyo, anasema kuwa sheria hiyo inawafanya polisi kuwa juu ya sheria, ingawa tangu zamani polisi wako juu ya sheria.

Kwa upande mwingine Lidetu Ayalew, kiongozi wa chama kingine cha upinzani cha Ethiopian Democtaric Party, ambacho pia kinaipinga sheria hiyo, anaamini kuwa kuna haja ya kuwa na sheria ya aina fulani inayopinga ugaidi kwa sababu nchi hiyo imekuwa ikiathirika na matukio kadhaa ya vitendo vya kigaidi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (IPS)

Mhariri: Othman Miraji

 • Tarehe 24.07.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Iwyt
 • Tarehe 24.07.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Iwyt

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com