1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ebrahim Raisi aapishwa kama rais wa Iran

Tatu Karema
5 Agosti 2021

Raisi ameapishwa kama rais wa nane wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hatua hiyo inaziweka nguzo tatu za serikali za ofisi ya rais, bunge na mahakama chini ya uongozi wa wahafidhina wenye msimamo mkali.

https://p.dw.com/p/3ybE2
Ibrahim Raisi
Picha: Mizan

Baada ya kuapishwa kwake, Raisi amesema kuwa anajitolea kwa utumishi wa raia wa nchi hiyo, hadhi ya taifa hilo, uenezaji wa dini na maadili, na uungaji mkono wa ukweli na haki. Raisi anachukuwa uongozi huo kutoka kwa kiongozi aliyekuwa na siasa za msimamo wa wastani Hassan Rouhani ambaye ufanisi wake mkubwa wakati wa uongozi wake wa mihula miwili ulikuwa mkataba wa nyuklia wamwaka 2015 kati ya Jamhuri hiyo ya kiislamu na mataifa sita yenye uwezo mkubwa zaidi duniani.

Wakati wa hafla ya kutawazwa kwake siku ya Jumanne na kiongozi mkuu wa taifa hilo Ayatollah Ali Khamenei, Raisi alisema kuwa masuala atakayoyapa kipaombele ni kukabiliana na ufisadi, mgogoro wa kiuchumi wa taifa hilo pamoja na kupanda kwa gharama ya maisha. Pia alitaja kuwa anataka vikwazo vya kidhalimu vilivyowekwa na Marekani kwasababu ya mkataba wa nyuklia wa Iran kuondolewa.

Iran Tehran | Iranischer Präsident | Hassan Rouhani
Hassan Rouhani- Rais aliyekuwa rais wa IranPicha: Iranian Presidency/Anadolu Agency/picture alliance

Swali kuu kutoka kwa watu wengi nje ya taifa hilo limekuwa ni athari ya mabadiliko hayo kuelekea kwa upande wa kihafidhina zaidi katika hali ya mazungumzo yasio ya moja kwa moja na Marekani katika kuyarejesha mataifa hayo mawili katika mkataba huo wa nyuklia wa mwaka 2015 unaolenga kuizuia Iran kutengeza silaha za nyuklia ili kubadilishana na kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi. Raisi pia alisema kwamba wanaamini kuwa nafasi ya kiuchumi ya raia nchini humo ni duni kwasababu ya uhasama wa maadui zao na pia kwasababu ya mapungufu ndani ya taifa hilo.

Wakati huo huo, mvutano katika kanda hiyo unaendelea kukithiri huku kiongozi wa jeshi la mapinduzi nchini humo Jenerali Hussein Salami, leo akizonya Israeli na mataifa ya Magharibi dhidi ya kujaribu kuidhalilisha Iran na kusema kuwa wale wote wanayoitishia wanapaswa kufahamu kuhusu matokeo hatari ya matamshi yao na kuchunga wanachokisema. Matamshi ya jenerali huyo yanafuatia shambulio la ndege isizoendeshwa na rubani dhidi ya meli ya mafuta inayoendeshwa na Uingereza katika ghuba ya Uajemi wiki moja iliyopita. Iran ililaumiwa na serikali za Marekani, Uingereza na Israeli kwa shambulio hilo lililosababisha mauaji ya wafanyakazi wawili wa meli hiyo.

Iran imekanusha kuhusika katika shambulio hilo na kutaja shtuma hizo kuwa uchokozi wa kisiasa. Wizara ya mambo ya nje nchini humo imeonya kuwa iwapo matukio hayo yatahatarisha usalama wa taifa hilo, itachukuwa hatua zinazostahili.