1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Khamenei amthibitisha rasmi rais Iran

3 Agosti 2021

Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amemtambulisha rasmi Ebrahim Raisi kuwa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran rais huyo mteule ataapishwa rasmi bungeni siku ya Alhamisi.

https://p.dw.com/p/3yT7l
Teheran, Iran | Ebrahim Raisi | Inauguration
Picha: FARARU

Rais huyo mteule ameahidi kuchukua hatua za kuondoa vikwazo vilivyowekwa na Marekani. Soma zaidi Mhafidhina Ebrahim Raisi ashinda kura ya urais Iran

Raisi, ambaye mwenyewe amewekewa vikwazo Marekani kwa madai ya ukiukaji wa haki za binadamu wakati akihudumu kama jaji mkuu, ameahidi kuboresha hali ya maisha ya Iran ambayo imekuwa mbaya zaidi tangu 2018 wakati Washington ilipoliwekea tena vikwazo taifa hilo la Kiislamu baada ya kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia. soma Rais wa Iran autetea mkataba wa nyuklia

Kwa mujibu wa katiba ya Iran, Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei ndiye muamuzi mkuu wa mambo yote ya kitaifa. Kuingia madarakani kwa Raisi anayeelemea siasa kali za kihafidhina za Iran kunaangaliwa kama ishara ya kuondoa ushawishi wa kusimamia sera za mtangulizi wake, Hassan Rouhani, mwenye msimamo wa wastani. Soma Iran yaandaa uchaguzi wa rais

Raisi ataapishwa Alhamisi

Teheran, Iran | Ebrahim Raisi | neu gewählter Präsident
Ebrahim Raisi Picha: Vahid Salemi/AP Photo/picture alliance

Raisi ataapishwa siku ya Alhamisi na kisha atapewa wiki moja kuwasilisha baraza lake la mawaziri bungeni kwa kura ya imani.

Khamenei alimteua Raisi kuendesha idara ya mahakama mnamo 2019, na miezi mitatu baadaye aliwekewa vikwazo na Marekani kwa madai ya kuhusika na mauwaji ya maelfu ya wafungwa wa kisiasa mnamo 1988. Iran haijawahi kukubali kuhusika na mauaji hayo.

Raisi anachukua nafasi ya Rouhani, ambaye mafanikio yake ya kihistoria yalikuwa makubaliano ya nyuklia ya 2015 kati ya Iran na Mataifa sita yenye nguvu ulimwenguni. soma Rais mteule wa Iran Ebrahim Raisi asema hatakutana na Rais wa Marekani Joe Biden

Muelekeo wa utawala wake

Teheran, Iran | Ebrahim Raisi | neu gewählter Präsident
Picha: Maryam Rahmanian/newsroom/picture alliance

Katika hotuba yake Raisi amesema "Demokrasia ya kidini ilikuja katika nchi hii zaidi ya miaka 40 iliyopita, kupitia mwongozo wa kiongozi wetu marehemu Ayatollah Ruhollah Khomeini na kupitia juhudi za taifa letu kubwa na lenye dhamana. Tumeuonyesha ulimwengu mtindo mpya wa utawala, ambayo dini inasimama pamoja na mambo ya sasa, sayansi inasimama katika kiwango sawa na maadili, suala la haki lina thamani sawa na maendeleo, utu na ustawi viko katika kiwango sawa. kila mtu anaweza kuona uhusiano wa kiroho na maisha ya wanadamu wa kisasa. "

Kuanzia mwanzo wa madaraka yake, Raisi atalazimika kushughulikia mazungumzo ya  kufufua makubaliano ya nyuklia ambayo rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, alijiondoa na kuiwekea tena vikwazo Iran.

Utawala wa Raisi utaimarisha mamlaka mikononi mwa wahafidhina kufuatia ushindi wao wa uchaguzi wa bunge wa mwaka 2020, ambao unakosolewa kwa kuwazuwia wagombea wanaopendelea mabadiliko na wale wanaofuata siasa za mrengo wa kati.

 

Vyanzo/dpa/AFP