China yaendelea na luteka yake ya kijeshi karibu na Taiwan
30 Desemba 2025
Kulingana na data za serikali, idadi kubwa ya ndege za kivita za china zinawakilisha idadi ya pili kubwa kuwahi kushuhudiwa karibu na anga ya Taiwan. Mwezi Oktoba mwaka 2024 wakati wa zoezi jengine la kijeshi la "Joint Sword 2024B" ndege 153 zilirekodiwa. Kando na hilo Taiwan pia imegundua meli 14 za kivita za China, meli nyengine za taifa hilo pamoja na puto moja.
Wizara ya ulinzi ya Taiwan, imesema China imezindua luteka ya kijeshi karibu na kisiwa chakeikitumia silaha nzito za moto ikilenga maeneo ya Bandari, Kaskazini na Kusini Magharibi mwa Taiwan.
Jeshi la kisiwa hicho lilijibu zoezi hilo kwa kutumia mifumo ya silaha za moto. Waziri wa ulinzi Wellington Koo, amesema hatua za China alizoziita za kichokozi na za kizembe sio tu zinahatarisha amani na uthabiti wa kikanda lakini pia zinatishia usalama na kusamabaratisha biashara, safari za angani na majini.
Nae rais wa Taiwan Lai Ching-te amesema shinikizo za kijeshi zinazofanywa katika siku za hivi karibuni kutoka China sio jambo linalopaswa kufanywa na dola linalojiona kuwa moja ya nchi zilizo na nguvu duniani.
Rais huyo ameandika katika mtandao wake wa kijamii kuwa katika kulinda amani katika mlango wa bahari wa Tiwan na katika eneo la Indo Pasifiki ni jambo matarajio ya kila mmoja katika Jumuiya ya Kimataifa na ni jambo ambalo Taiwan inaliheshimu kama mdau wa kikanda.
Chinailianzisha mazoezi hayo ya kijeshi Jana Jumatatu (29.12.2025) yaliyoitwa "Justice Mission 2025"
linalojumuisha meli za kivita, wapiganaji, makombora na madroni. Mazoezi hayo yanalenga kuonesha utayari wa kukabiliana kupitia majini, kukizingira kisiwa hicho hasa katika bandari na maeneo yake muhimu. Jeshi la China lilitoa onyo kwamba kwa sababu ya usalama, hakuna meli yoyote inayotakiwa kupita katika mlango wa bahari wa Taiwan.
Beijing inadai Taiwan kuwa sehemu ya eneo lake na imekataa kuondoa uwezekano kwamba itatumia hatua za kijeshi kukidhibiti kikamilifu kisiwa hicho. Hatua ya hivi karibuni iliyokosolewa na China ni Marekani ambayo ni mshirika mkubwa wa Taiwan, kuiuzia kiwango kikubwa cha silaha.