China imeyataja maandamano ya Hong Kong sio halali | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.09.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

China imeyataja maandamano ya Hong Kong sio halali

China imeyataja maandamano makubwa yanayofanyika Hong Kong kutaka mageuzi ya kidemokrasia kuwa sio halali na kusisitiza serikali ya China haitaitikia matwaka ya waandamanaji hao.

Maelfu ya waandamanaji ambao wamekita kambi katikati ya mji wa Hong Kong kwa siku kadhaa sasa,wameapa kutositisha maandamano hayo hadi serikali kuu ya China iwape uhuru kamili wa kuendesha chaguzi zao kwa njia ya kidemokrasia.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Hua Chun-Ying amesema katika mkutano na wanahabari kuwa kumekuwa na mkusanyiko usio halali Hong Kong ambao ulianza tangu Jumapili na kufuatiwa na vitendo vilivyo kinyume na sheria.

China ina imani na serikali ya Hong Kong

Hua amesema wana imani na wanaiunga mkono serikali ya Hong Kong katika jinsi inavyoshughulikia suala hilo la maandamano baada ya kiongozi wa Hong Kong Leung Chun-Ying kusema maandamano hayo yamevuka mipaka.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya China Hua Chunying

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya China Hua Chunying

Leung amewataka waandalizi wa maandamano hayo kuyasitishwa mara moja na kusema vitendo ambavyo ni kinyume na sheria havitaifanya serikali kuu ya China kubadili uamuzi wake kuhusu sheria za chaguzi za Hong Kong.

Kiongozi wa China, Xi Jinping hajatoa tamko lolote hadharani kuhusiana na maandamano hayo makubwa ya Hong Kong yanayotafuta kupanuliwa kwa mfumo mpana zaidi wa demokrasia na mageuzi ya mfumo wa kupiga kura na amesalia kimya huku yeye pamoja na maafisa wengine wakuu wa chama cha kikomunisti wakjitoa vikapu vya maua katika ukumbi wa Tiananmen hii leo kuadhimisha siku ya kwanza ya sherehe za kuwakumbuka mashujaa wa China.

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron amesema leo anatiwa wasiwasi mkubwa na makabiliano yanayozuka kati ya maelfu ya waandamanaji na polisi mjini Hong Kong na kuongeza anatumai mzozo uliopo utasuluhishwa.

Nchi za kigeni zatiwa wasiwasi na makabiliano

Marekani hapo jana iliwataka viongozi wa Hong Kong kuonyesha kujizuia katika jinsi inavyoyashughulikia maandamano hayo na kusema inaunga mkono haki ya kupiga kura kwa wote hata katika maeneo ambayo yako katika himaya ya China.

Polisi Hong ikikabiliana na waandamanaji

Polisi Hong Kong ikikabiliana na waandamanaji

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China amezishutumu nchi za kigeni zinazotoa maoni yao kuhusu maandamano hayo na kusema masuala ya Hong Kong yako chini ya China na kuzionya nchi za kigeni dhidi ya kuingilia masuala ya ndani ya China kwa njia yoyote.

Maandamano hayo ya Hong Kong ya kudai mageuzi ya kidemokrasia yamepata uungwaji mkono kutoka nchi za nje tangu yaliposhika kasi mwishoni mwa juma lililopita.

Watu wamejitokeza kufanya maandamano ya kuwaunga waandamanaji wa Hong nchini Taiwan, Malaysia, Austaralia ,Uingereza na Marekani na maandamano zaidi yanapangwa kufanyika New Zealand, Japan, Ujerumani na Switzerland.

Mwandishi:Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com