Bunge la Seneti lakataa kifungu cha ubaguzi wa kibiashara Marekani | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 05.02.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Bunge la Seneti lakataa kifungu cha ubaguzi wa kibiashara Marekani

Bunge la seneti la Marekani jana lilipiga kura kutoridhia kuwepo kwa kipengee kinachosema ''Buy America, kwenye mpango wa kufufua uchumi wa Marekani wenye thamani ya dola billioni 900.

Rais wa Marekani Barack Obama

Rais wa Marekani Barack Obama

Kipengee hicho kinataka makampuni pamoja na viwanda vitakavyofaidika na fedha hizo kununua malighafi kutoka humo humo Marekani.


Hatua ya bunge la Marekani kupiga kura kutaka kuondolewa kwa kipengee hicho inafuatia, wasiwasi uliooneshwa na rais mpya wa Marekani Barack Obama ya kwamba lugha hiyo ya ''Nunua Marekani'' inaweza kuwa chanzo cha vita vya kibiashara duniani.


Maseneta walipiga kura kutaka kulainishwa kwa lugha iliyotumika katika kifungu hicho na kwamba iendane na matakwa ya Marekani chini ya makubaliano ya biashara ya kimataifa.


Mabadiliko hayo yanazipa ahueni nchi za Canada, Mexico, Umoja wa Ulaya na washirika wengine wakubwa kibiashara wa Marekani ya kwamba hazitabanwa na matakwa ya mpango huo wa kufufua uchumi wa Marekani unaotaka miradi yote itakayofaidika na fedha hizo kutumia malighafi kutoka Marekani. Lakini kwa kura hiyo ya seneti sasa nchi zenye makubaliano ya kibiashara na Marekani hazibanwi na kifungu hicho.


Baraza la wawakilishi lilipitisha mpango huo wa kufufua uchumi kikiwemo kipengee hicho cha Buy America, ambapo katika bunge la Seneti , aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Republican Seneta John McCain wa jimbo la Arizona aliwataka maseneta wenzake kupitisha mpango huo pamoja na kipengee hicho lakini walikataa kwa kura 65 dhidi ya 31.


Kamati ya dharura inayohusika na biashara nchini Marekani pamoja na muungano wa zaidi ya vyama 125 vya biashara nchini humo ilionya dhidi ya kipengee hicho ya kwamba kitapelekea uhasama wa kibiashara duniani.


Marekani imo katika makubaliano ya biashara huru Amerika Kaskazini, North America Free Trade Agreement, pamoja na Shirikisho la Biashara Duniani, makubaliano ambayo yanaitaka kushirikiana kibiashara na nchi kama Canada, Japan, Mexico na Umoja wa Ulaya kwa kufungua soko lake kwa nchi hizo, ambapo nayo pia ina nafasi kama hiyo kwa nchi hizo.


Seneta Byron Dorgan, kutoka Dakota ya Kaskazini amesema kuwa wale wote wanaoupigia upatu mpango huo wa Buy America wanataka wananchi wa Marekani wafaidike na fedha zitakazotolewa kwa miradi na viwanda.


Wakati huo huo rais Barack Obama amezuia malipo ya malimbikizo ya dola laki tano kwa mwaka ambayo walikuwa walipwe wakurugenzi wakuu wa mashirika yatakayopata fedha za mpango huo wa kufufua uchumi, akisema hayo ni matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi.


Rais Obama amesema kuwa wiki ijayo hatua zaidi zitaainishwa katika kukabiliana na shutuma zinazoikabili sekta ya fedha nchini Marekani kwa matumizi mabaya ya mabilioni ya dola ya fedha za umma.


Waziri wa fedha Timothy Geithner amesema kuwa wiki ijayo atatoa maelekezo ya jinsi gani fedha hizo za kufufua uchumi zitakavyotumika.


Hatua hiyo ya Rais Obama kuzuia wakuu wa mashirika kulipwa kiasi kikubwa cha fedha imepongezwa na wengi, lakini kwa upande wa makampuni hayo wamelaumu hatua hiyo wakisema kuwa imechukuliwa kisiasa.


 • Tarehe 05.02.2009
 • Mwandishi Aboubakary Jumaa Liongo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GnZD
 • Tarehe 05.02.2009
 • Mwandishi Aboubakary Jumaa Liongo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GnZD
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com