1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yapitisha mpango wa sheria ya usalama mjini Hong Kong

Lilian Mtono
28 Mei 2020

Bunge la China leo limepitisha mipango ya kutungwa sheria mpya ya usalama wa taifa mjini Hong Kong ambayo wakosoaji wake wanasema itavuruga uhuru na hadhi ya mji huo.

https://p.dw.com/p/3csbl
China Nationaler Volkskongress | Abstimmung Sicherheitsgesetz Hongkong
Picha: Reuters/C. G. Rawlins

Zaidi ya wajumbe 2,800 wa Baraza la Taifa la Umma wa China wamepiga kura kuunga mkono pendekezo la kutungwa sheria hiyo itakayowaadhibu wanaojihusisha na kutaka kujitenga, kudhoofisha nguvu ya dola, ugaidi na vitendo vyote vinavyotishia usalama wa taifa.

Tangazo la matokeo hayo lilikaribishwa na shwange kutoka kwa wajumbe na taarifa zimesema ni mjumbe mmoja pekee ndiye amepinga pendekezo hilo na wengine sita hawakupiga kura.

Mipango ya kutunga sheria hiyo imezusha ukosoaji mkubwa kutoka mataifa ya kigeni, wawekezaji na vuguvugu la kudai demokrasia mjini Hong Kong wanaosema China inaondoa misingi yote ya uhuru iliyoahidi wakati wa mkataba wa kuuchukua tena mji huo mwaka 1997.

Kulingana na muswada wa pendekezo hilo uliochapishwa wiki iliyopita, sheria hiyo itaruhusu idara za usalama la China Bara kufanya shughuli zake kwa uwazi katika jiji hilo.

China Bara imekuwa ikitumia mara kwa mara sheria ya kitaifa ya usalama kuwakamata wanaharakati, waandishi wa habari na wanasheria bila ya kuwafungulia mashitaka ama kuwapatia fursa ya kupata mawakili.

 Soma Zaidi: Polisi Hong Kong wapambana na waandamanaji