1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunduki aiana ya Kalashnikov yaendelea kuhatarisha maisha ya wengi.

jane nyingi/AFP10 Novemba 2009

Huku akikaribia kutimia umri wa miaka 90, aliyetengeneza bunduki aina ya Kalashnikov,Mikhail Kalashnikov, raia wa Urusi, hivi kwa sasa anajuta kutokana na wazo lake.

https://p.dw.com/p/KSwJ
Wapiganaji kutoka Ossetia Kusini wakiwa na bunduki aiana ya KalashnikovPicha: AP

Silaha hiyo, ambayo uliundwa mwaka 1947, imekuwa chaguo la makundi ya wahalifu, wakiwemo wapiganaji na makundi ya waasi nchini Liberia na Afghanistan. Huyu hapa Othman Miraji na ripoti kamili.

“Ni uchungu ninapowaona wahalifu wa kila aina wakifanya mashambulio wakitumia silaha niliyoibuni„ Mikhail Kalashnikov aliuambia mkutano wa wafanya biashara wa silaha nchini Urusi, katika hotuba yake iliyokuwa imerekodiwa kwenye kanda ya video. Kutokana na kazi zake nchini Urusi, Kalashnikov ni shujaa na sherehe ya kifahari kuadhimisha miaka 90 tangu azaliwe inatazamiwa kuandaliwa na serikali mwezi ujao. Huku uvumbuzi wake ukipokelewa kwa mikono miwili na wanamapinduzi kutoka mabara ya Asia na Amerika ya Kusini, kwa wapinzani wao kutoka magharibi,alikuwa muasisi wa silaha ya mauji na kusababisha umwagikaji damu.

Kalashnikov alieleza wazi katika hotuba yake hiyo kupitia ukanda wa video kuwa hakufikiria bunduki kama hiyo ingeenea kote ulimwenguni.“Nilibuni silaha hii ili kuilinda nchi yangu, alisema Kalashnikov huku akionekana dhaifu. Bunduki ya Kalashnikov iliundwa muda mfupi baada ya vita vikuu vya pili vya dunia ili kutumika katika mazingira magumu waliokuwemo wanajeshi wa kisovieti. Kalashnikov ni rahisi kuitengeneza na kuitunza, na imekuwa moja ya silaha ambazo soko lake limeongezeka. Bunduki hiyo sasa inatumika katika mataifa 55 na watoto wanaozaliwa katika baadhi ya mataifa wanapewa jina Kalash, kutokana na jina la bunduki hiyo ya Kalashnikov

Japokuwa karibu bunduki millioni 100 aina ya Kalashnikov zimetengenzwa katika muda wa miaka 60 na kutumika, ni nusu yake tu zilizo na leseni na pia kufikia viwango vinavyohitajika na Urusi. Anatoly Isaikin, mkuu wa shirika pekee nchini Urusi linalosafirisha silaha katika nchi za nje, Rosoboron export, amesema Kalashnikov bandia zimeharibu jina la chapa ya bunduki hiyo kwa kuwa nyingi zinauzwa katika maeneo ya vita.

Kampuni hiyo inafanya mashauri ya kuweko makubaliano na viwanda vya kigeni vinavyotengeneza bunduki hiyo ili kuilinda na pia kulinda silaha nyingine kutoka Urusi. Alisema viwanda 30 vya kigeni kwa sasa vinatengeneza bunduki hiyo aina ya Kalashnikov. Wakati wa enzi za kisovieti, Urusi mara kwa mara ilikuwa inatia saini makubalino ya miaka 25 ya leseni za silaha na nchi za mashariki mwa bara la Ulaya ili kuziruhusu kutengeneza kalashnikov. Hivi sasa makubalino hayo muda wake umekwisha. Vladmir Grodetsky, kiongozi wa Ishmash, alisema kufikia sasa Urusi imetia saini makubalino na Venezuela kujenga kiwanda cha kutengeneza bunduki hiyo aina ya Kalashnikov na shughuli zake zinatazamiwa kuanza katika muda wa miaka miwili ijayo.

Alisema mataifa mengine, ikiwemo China na nchi kadhaa za magharibi mwa bara la Ulaya, zipo tayari kwa mazungumzo ili kuheshimu haki miliki ya bunduki ya aina ya Kalashnikov, lakini haya yote lazima yafanyika na serikali. Licha ya kuingia katika soko bunduki bandia aina ya Kalashnikov na kuiharibia ubora wake, Urusi bado inaziuza katika bei ambayo ni asilimia 50 chini, kuliko vile mtu angelipia bunduki aina ya Kimarekani, M-16.

Mwandishi:Jane Nyingi

Mhariri:Othman Miraji