Brown na Sarkozy wapania kuhusu amani ya Darfur | Matukio ya Kisiasa | DW | 31.08.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Brown na Sarkozy wapania kuhusu amani ya Darfur

Katika kile kinachoonekana kuwa ni shinikizo zaidi dhidi ya Sudan, waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown na Rais wa Ufaransa Nikolas Sarkozy, wameungana pamoja kuzipa msukumo juhudi za kuleta amani katika jimbo la Darfur, wakiionya serikali ya Sudan juu ya uwezekano wa kuekewa vikwazo iwapo itakwamisha juhudi hizo.

Wanajeshi wa kikosi cha Umoja wa Afrika huko Darfur(AMIS) ambacho kimekua dhaifu kutokana na uhaba wa nyenzo .

Wanajeshi wa kikosi cha Umoja wa Afrika huko Darfur(AMIS) ambacho kimekua dhaifu kutokana na uhaba wa nyenzo .

Viongozi hao wawili wameelezea msimamo wao katika makala iliochapishwa leo na gazeti la The Times la mjini London wakiitaka pia jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi zake kuleta ufumbuzi wa mgogoro wa Darfur.Brown na Sarkozy wameandika,”Bado kuna mwanya kati ya juhudi za kuishawishi jumuiya ya kimataifa na hali tete iliobakia Darfur kwenyewe.”

Wamesema kwamba ni usimamishaji mapigano tu, kuweko kwa kikosi cha kusimamia amani, ujenzi mpya wa uchumi na kitisho cha vikwazo, yatakayopweza kuleta suluhisho la kisiasa katika jimbo hilo.Waziri mkuu Brown wa Uingeereza na Rais Sarkozy wa wameahidi kuongeza juhudi zao maradufu ili kupiga hatua zaidi ya maendeleo, wakisisitiza kwamba hali ya sasa haikubaliki hata kidogo.

Makala yao imechapishwa kabla ya kutumwa kikosi cha pamoja cha Umoja wa mataifa na Umoja wa Afrika cha wanajeshi karibu 26,000 kilichokubaliwa na baraza la usalama la umoja wa mataifa mwezi uliopita,baada ya miezi kadhaa ya harakati za kidiplomasia kumshawishi Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir.

Kikosi kamili kitakachochukua nafasi ya kile cha sasa cha umoja wa Afrika ambacho ni dhaifu, hakitarajiwi kuweko Darfur kabla ya katikati ya mwaka ujao 2008. Umoja wa mataifa umesema kwamba zaidi ya watu 200,000 wamekufa na zaidi ya milioni mbili wamelazimika kutawanyika kutokana na mgogoro huo wa Darfur unaoendelea kwa miaka minne sasa.

Sarkozy na Brown wameandika katika makala yao kwamba mnamo siku zijazo waziri mdogo anayehusika na masuala ya kigeni wa Ufaransa na mwanaharakati wa haki za binaadamu Rama Yade pamoja ana waziri mdogo wa mashauri ya kigeni wa Uingereza Lord Mark Malloch-Brown wataizuru Sudan ikiwa ni pamoja na jimbo la Darfur kama sehemu ya shinikizo la kidiplomasia kulpata usimamishaji mapigano wa haraka.

Waziri mkuu wa Uingereza na Rais wa Ufaransa wametoa wito wa suluhisho la kisiasa litakaloliruhusu jimbo la Darfur kushiriki katika uchaguzi wa taifa nchini Sudan 2009 na kusema kwamba kama hakuna hatua ya kutosha ya maendeleo itakayopigwa kuhusu usalama katika jimbo hilo, ikiwa ni pamoja na usimamishaji mapigano, utaratibu wa kisiasa na usalama kwa shughuli za usambazaji misaada, basi vikwazo dhidi ya utawala mjini Khartoum vitazingatiwa. Uingereza na Ufaransa ni wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa mataifa.

Wakati huo huo katika ripoti yake iliotolewa jana, Umoja wa amataiafa umesema kwamba muda uliowekwa wa Agosti 31 kwa ajili ya kuchangia wanajeshi katika kikosi cha kimataifa hauna budi kurefushwa kwa sababu bado kuna ukosefu kuchangia baadhi ya mahitaji muhimu ya kijeshi. Akitoa ripoti hiyo katibu mkuu Ban Ki-moon hakutaja tarehe mpya ya muda wa kuchangia wanajeshi wapatao 19,555 kusaidia kumaliza mapigano huko Darfur. Alisema kuna mapendekezo ya kutosha ya kuchangia polisi wa kiraia 6,000 walioombwa , lakini ni nchi chache zilizo tayari kufanya hivyo.

Umoja wa mataifa unasema una uhaba wa ndege za uchukuzi na wapangaji mikakati wanaohitajika ili kikosi kipya cha wanajeshi 26,000 kinachotarajiwa kupelekwa Darfur kiwajibike ipasavyo.

 • Tarehe 31.08.2007
 • Mwandishi Mohammed Abdul-Rahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH8f
 • Tarehe 31.08.2007
 • Mwandishi Mohammed Abdul-Rahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH8f

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com