Bolt atwaa medali yake ya tisa ya Olimpiki | Michezo | DW | 20.08.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Bolt atwaa medali yake ya tisa ya Olimpiki

Mwanariadha wa Jamaica, Usain Bolt, ameshinda kwa mara ya tatu mfululizo kwenye Michezo ya Olimpiki ya Rio 2016, akijipatia medali yake ya tisa ya dhahabu wakati akiiaga rasmi michezo hiyo ya kimataifa.

Mshindi wa mara tisa wa michezo ya Olimpiki, Usain Bolt wa Jamaica.

Mshindi wa medali tisa za dhahabu za michezo ya Olimpiki, Usain Bolt wa Jamaica.

Akiwa kwenye timu moja na Asafa Powell, Yohan Blake na Nickel Ashmeade katika mbio za kupokezana vijiti za mita 100, Bolt ameshinda kwa kukimbia kwa sekunde 37.27, huu ukiwa mchezo wake wa mwisho kwenye mashindano haya maarufu duniani.

Timu ya Japan iliambulia medani ya fedha ikiwa nayo imeweka rikodi ya bara la Asia kwa kukimbia kwa sekunde 37.60 na Canada kujitwalia medali ya shaba kwa kukimbia kwa dakika 37.64. Hii ni baada ya timu ya Marekani, ambayo ndiyo iliyokuwa ichukuwe nafasi ya tatu, kufutwa.

Bolt alishashida mbio za mita 100, mita 200 na mbio za kupokezana vijiti kwa mita 100 katika Olimpiki za Beijing 2008 na London 2012, na sasa ana rikodi ya dunia kwa michezo yote mitatu.

Bingwa huyo wa dunia ambaye pia ana medali 11 nyengine, sasa anashabihiana na Mmarekani Carl Lewis mwenye medali tisa.

Vivian Jepkemoi Cheruiyot wa Kenya aliyeshinda mbio za mita 5,000.

Vivian Jepkemoi Cheruiyot wa Kenya aliyeshinda mbio za mita 5,000.

Lewis alishinda mbio za mita 100, mita 200, mbio za mita 100 za kupokezana vijiti na pia kuruka viunzi mnamo mwaka 1984, akiongeza pia dhahabu nyengine tatu kwenye viunzi, mbili kwenye mbio za kupokezana vijiti na moja kwenye mbio za mita 100 katika mashindano ya baadaye ya Olimpiki.

Bolt anayetimiza miaka 30 kesho Jumapili (21 Agosti), alisema baada ya ushindi wake wa mita 200 siku ya Alhamisi kuwa Rio itakuwa Olimpiki yake ya mwisho, ingawa bado anapanga kushiriki michezo ya dunia jijini London mwakani.

Mkenya Cheruiyot ashinda mita 5,000

Mkenya Vivian Cheruiyot akijitwalia medali ya dhahabu baada ya kushinda mbio za mita 5,000 akimshinda kwa mbali aliyekuwa anashikilia rikodi ya mbio hizo, Almaz Ayana wa Ethiopia.

Awali Ayana, ambaye pia alishajishindia medali ya dhahabu siku ya Jumamosi kwa kuweka rikodi katika mbio za mita 10,000, alikuwa anaongoza hadi wakiwa wamefikia mita 1,800 akiwa mbele kwa takribani mita 40, lakini Cheruiyot na Mkenya mwenzake, Hellen Obiri, wakasonga mbele na kumpita na kumuacha akiwa nyuma yao, mita 600 kabla ya mchezo kumalizika.

Cheruiyot alitumia dakika 14 na sekunde 26.17, akimtangulia Obiri kwa sekunde tatu na huku bingwa wa dunia Ayana akipata medani ya shaba kwa kuwa nyuma kwa sekunde nane.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa
Mhariri: Sudi Mnette